Nani mkali: Simba wawili kukabiliana fainali AFCON 2025

Senegal na Morocco itapambana katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) mwishoni mwa wiki hii.

By
Morocco ikisherehekea ushindi wao dhidi ya Nigeria kwenye nusu fainali. /cafonline

Mashindano hayo yaliyoanza kabla ya mwisho wa mwaka uliopita na yamekuwa na burudani si haba huku yakikaribia kufikia tamati mjini Rabat, Morocco ambapo mshindi mwingine tofauti atabeba taji baada ya bingwa Cote d’Ivoire kufungishwa virago katika hatua ya robo fainali.

Siku ya Jumatano Senegal iliwafunga Misri huku Morocco ikimaliza wababe dhidi ya Nigeria na kuthibitisha ratiba nyingine kali ya mataifa mawili mahiri wa soka barani Afrika.

Wenyeji Morocco walihitaji matuta kuwaondoa Nigeria mjini Rabat Jumatano usiku.

Youssef En-Nesyri ndiye aliyefunga penati ya ushindi katika Uwanja wa Prince Moulay Abdellah na kuleta matumaini ya vijana wa Walid Regragui wanapoelekea kwenye fainali siku ya Jumapili.

Hii ni historia kwa Morocco ambayo inaingia fainali yake ya kwanza katika kipindi cha miaka 21.