Uwanja wa ndege wa Arusha nchini Tanzania, unatarajiwa kuanza kutoa huduma saa 24, kuanzia mwezi Agosti mwaka huu baada ya kukamilika kwa mradi wa usimikaji wa taa za kuongozea ndege, maarufu kama “Airfield Ground Lighting” (AGL).
Akikagua maendeleo ya mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Abdul Mombokaleo, amesema kuwa ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilika kwa wakati huku viwango vya ubora na usalama vikizingatiwa.
"Kuanzishwa kwa huduma za ndege usiku na mchana katika uwanja wa ndege wa Arusha kutapanua uwezo wa kiwanja hiki kuhudumia safari nyingi zaidi, kuongeza usalama wa safari na kuwapa wawekezaji na watalii urahisi mkubwa wa kufika katika vivutio vya utalii vilivyopo Kaskazini mwa Tanzania," alieleza.
Uwanja wa ndege wa Arusha miongoni mwa viwanja muhimu vinavyohudumia sekta ya utalii nchini humo, na ni lango kuu kwa wasafiri wanaoelekea Hifadhi za Taifa za Serengeti, Ngorongoro, Tarangire, Ziwa Manyara na Mlima Kilimanjaro.
Maboresho hayo, pia yanatarajiwa kuongeza ushindani wa sekta ya anga na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha utalii barani Afrika.
Aidha maboresho hayo yanakuja wakati Mkoa wa Arusha ukijiandaa kupokea matukio makubwa ya kimataifa ikiwemo mashindano ya AFCON 2027 na mashindano ya mlimbwende wa dunia.













