| Swahili
AFRIKA
1 dk kusoma
Tanzania yawaasa wasanii na watengeneza maudhui kulinda maadili ya jamii
Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa sekta ya ubunifu kupitia mikopo na programu mbalimbali za kuwawezesha wasanii na wabunifu nchini.
Tanzania yawaasa wasanii na watengeneza maudhui kulinda maadili ya jamii
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa, amewataka wasanii na watengenezaji wa maudhui nchini humo, kutumia vipaji vyao kujenga maadili mema, kuhamasisha uzalendo na kuleta maendeleo ya jamii kupitia kazi zao.

Akizungumza katika hafla ya kumpongeza mtengenezaji wa maudhui Abdul Hussein Chacha (Headmaster), Msigwa amesema serikali ya Tanzania itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa sekta ya ubunifu kupitia mikopo na programu mbalimbali za kuwawezesha wasanii na wabunifu nchini humo.

Aidha, amesema Mfuko wa Utamaduni na Sanaa hadi sasa umetoa zaidi ya Shilingi bilioni 14 kwa wasanii, huku zaidi ya Shilingi bilioni 3 zikielekezwa kwa watengenezaji wa maudhui ya mtandaoni ili kuboresha ubora wa kazi zao na kuongeza ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi hiyo.

Katika hafla hiyo, Abdul Hussein Chacha alitunukiwa Shilingi milioni 5, kadi ya uanachama wa NSSF, pamoja na msimbo papo wa kumwezesha kutangaza na kuuza kazi zake katika masoko ya ndani na kimataifa.

CHANZO:TRT Afrika Swahili