Watu watatu wamefariki kwenye meli ya kitalii, Shirikia la Afya Duniani (WHO) limesema, huku likithibitisha kifo cha mtu mmoja kufuatia mlipuko wa virusi vya Hantavirus.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa maabara —ugonjwa huo kwa kawaida huambukizwa kwa binadamu kupitia panya.
Mlipuko huo ulitokea kwenye meli ya MV Hondius, iliyokuwa ikisafiri kutoka nchi ya Argentina kuelekea Cape Verde.
“Hadi sasa, kuna mtu mmoja ameambukizwa na virusi vya hantavirus iliyothibitishwa na maabara, watu wengine watano washukiwa pia kuambukizwa na virusi hivyo,” WHO ilisema.
Mgonjwa aliyekuwa akitibiwa jijini Johannesburg, Afrika Kusini alipimwa na kukutwa na hantavirus, aina ya virusi vinavyoweza kusababisha homa ya kuvuja damu na matatizo makubwa ya kupumua.
Uchunguzi unaendelea
"Maambukizi haya mara nyingi hutokana na hewa yenye chembechembe kutoka kwenye mkojo au kinyesi cha panya, ingawa ni nadra. Hantavirus pia inaweza kuenea kwa njia ya kuambukizana na kusababisha ugonjwa mkali katika mfumo wa upumuaji,” WHO ilibainisha.
Mhasiriwa wa kwanza, abiria mwenye umri wa miaka 70, alifariki dunia akiwa ndani ya meli.
Mke wake mwenye umri wa miaka 69 alihamishiwa Afrika Kusini, ambako naye pia alifariki dunia.
Mtu wa tatu aliyefariki mwili wake bado upo ndani ya meli hiyo.
Mashauriano yanaendelea kuamua iwapo abiria wengine wawili wagonjwa wanapaswa kuwekwa karantini Cape Verde kabla ya meli kuendelea na safari yake kuelekea Visiwa vya Canary vya Hispania.
MV Hondius, inayomilikiwa na kampuni ya Uholanzi ya Oceanwide Expeditions, inaweza kubeba takriban abiria 170 na wafanyakazi 70.











