Utajiri wa Afrika: Thieboudienne, mlo unaounganisha Senegal

Tafsiri yake ni "wali samaki," ambayo inaelezea kwa usahihi aina ya mlo huu. Asili yake inatokana na eneo la Saint-Louis, mji wa pwani kaskazini mwa Senegal unaojulikana kwa uhodari wake wa uvuvi.

By Coletta Wanjohi
Thieboudienne ina heshimiwa kote Senegal / Reuters

Sherehe bado zinaendelea nchini Senegal baada ya timu ya taifa kuchukua ubingwa wa AFCON 2025.

Senegal inapakana na Mauritania upande wa kaskazini, taifa la Mali sehemu ya mashariki, Guinea kusini mashariki na nchini Guinea-Bissau kwa upande wa kusini magharibi.

Ni nchi ya Afrika Magharibi inayojulikana kwa kuwa na utamaduni wenye utajiri mkubwa ambao unabaki thabiti licha ya usasa, na msingi wake ni vyakula vya kitamaduni.

Chakula maarufu kinachotambuliwa na kuheshimiwa kote nchini ni Ceebu Jen, ambacho inasemekana ilitoka kwa jamii za wavuvi kwenye Kisiwa cha Saint-Louis nchini Senegal.

Tafsiri yake ni "wali samaki," ambayo inaelezea kwa usahihi aina ya mlo huu.
Asili yake inatokana na eneo la Saint-Louis, mji wa pwani kaskazini mwa Senegal unaojulikana kwa uhodari wake wa uvuvi.

Mlo huo pia unaitwa Thieboudienne, kwa lugha ya Wolof, lugha inayozungumzwa zaidi nchini Senegal.

Chakula hiki kinachukuliwa kuwa cha kitaifa nchini humo, kinapendwa kote na ni sehemu ya maisha ya kila siku ya watu.

Kwa mapishi yake ya asili hupikwa katika chungu kimoja na aghalabu watu hula kwa pamoja. Ndani ya nchi pia kinajulikana kama benechin ikiwa na maana 'chungu kimoja' kwa lugha ya Wolof.

Chimbuko la Thieboudienne hasa ni matokeo ya umuhimu na ubunifu.

Wake za wavuvi enzi hizo walikuwa wakiandaa vyakula kutokana na kitoweo cha samaki waliovuliwa na waume zao siku hiyo pamoja na vyakula vingine vinavyopatikana nchini kama vile wali na mboga za majani.

Mchanganyiko huu mzuri wa ladha na viungo ndiyo unaunda mlo wa Thieboudienne.

Ingawa mapishi hutofautiana kutoka eneo moja hadi lingine, mlo kwa kawaida hutengenezwa kwa kitoweo cha samaki, wali, samaki waliokaushwa, vitoweo vingine vya kwenye maji kama konokono alafu kuungwa pamoja na vitunguu, vitunguu saumu, pilipili hoho, nyanya, karoti, biringanya, kabichi nyeupe, mihogo, viazi vitamu, na bamia.

Ubora wa samaki na mboga zinazotumika hubainisha umuhimu wa hafla au kiwango cha upendo ambacho mtu anacho kwa mgeni anayemuandalia mlo huu.

Uhodari wa upishi hurithishwa kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine.

Katika familia nyingi, watu hutumia mikono kula chakula hiki cha ceebu jen, ingawa vijiko au uma hutumiwa katika mikahawa. Kula pamoja kwenye sinia ni ishara ya umoja, heshima, na usawa. Kwa heshima mwenyeji humsogezeaa minofu mizuri ya samaki au mboga mgeni wake.

Ulaji wa mlo huo una sheria za kitamaduni.

Kwa mfano, ni marufuku kula ikiwa umeketi huku goti limenyanyuka, bakuli lazima lishikwe kwa mkono wa kushoto, na hata punji moja ya wali haitakiwi kuangushwa wakati wa kula.

Mlo wa ceebu jen na desturi zinazohusiana nayo zinatazamwa kama uthibitisho wa utambulisho wa watu wa Senegal.

Kwa hivyo ukiwa katika nchi hii ya Afrika magharibi iliyo kando ya pwani ya Bahari ya Atlantiki hakikisha umejaribu mlo huu wa kitaifa wenye ladha ya kipekee.