Mahakama ya Uchumi na Ufisadi ya nchini Zambia imeamuru kutaifishwa kwa mali zenye thamani ya shilingi milioni 24 za Zambia, zilizokuwa zikimilikiwa na Dalitso Lungu, ambaye ni mtoto wa zamani wa rais wa nchi hiyo, Edgar Lungu.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya kubainika kuwa mali hizo zilipatikana kwa njia za kihalifu.
Katika hukumu hiyo, mahakama hiyo ilisema kuwa, ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), mali hizo zilipatikana kwa njia isiyo halali, kulingana na Sheria ya Makosa ya Kihalifu namba 29 ya mwaka 2010.
Kulingana na hukumu hiyo, wahusika, ambao ni Dalitso Lungu na kampuni yake ya Saloid Traders Limited, walishindwa kutoa maelezo sahihi ya kuonesha namna ya walivyojipatia mali hizo.
Kati ya mali zitakazotaifishwa ni pamoja na magari 79, vipande 23 vya ardhi, biashara za nyumba, nyumba za makazi pamoja na vituo vya mafuta.
Mahakama hiyo, ilifanya rejea ya kazi alizowahi kufanya Lungu na mshahara aliokuwa akipata, na kubaini kuwa, aliwahi kufanya kazi katika kiwanda cha vinywaji cha Varun Beverages Zambia Limited mwaka 2012, akiwa anapokea Kwacha 5,407 za Zambia, katika kipindi cha miezi mitatu.
Pia, aliwahi kufanya kazi Mamlaka ya Mapato ya Zambia kwa kipindi cha miezi 34, akiwa anapata mshahara wa Kwacha 132,396 za Zambia.
Mahakama hiyo, ilihitimisha kuwa, mapato hayo hayakuwa sawa na mali ambazo alijapatia katika kipindi hicho.














