Papa Leo XIV kuzuru nchi ya Cameroon, Angola, Algeria na Guinea ya Ikweta

Papa Leo XIV atatembelea mataifa manne ya Afrika mwezi Aprili, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Vatican siku ya Jumatano, huku Algeria – ikiwa ni mara ya kwanza kwa papa kusafiri kwenda taifa hilo la Kiislamu la Afrika Kaskazini.

By
Papa Leo amepanga safari katika nchi nne za Afrika mnamo Aprili 2026. / / Reuters

Vatican ilitangaza mfululizo wa ziara za kimataifa katika miezi ijayo kwa kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki, aliyechaguliwa mwaka jana, ikiwemo safari za kwenda Hispania na Monaco.

Ziara ya Papa Leo inatarajiwa kujikita katika mazungumzo ya kidini. Mnamo Disemba, Papa alisema kuwa ziara ya Algeria itakuwa fursa ya kuimarisha “mazungumzo ya kidini kati ya Wakristo na Waislamu.”

Ziara za Cameroon, Angola na Guinea ya Ikweta

Algeria pia ni mahali alipozaliwa St Augustine of Hippo wa karne ya tano. Papa ni wa Utawa wa Waagustino (Augustinian), iliyoanzishwa katika karne ya 13.

St. Augustino (354–430), mmoja wa wanafalsafa na wanateolojia wakubwa wa Ukristo, alitoka katika eneo la sasa la Souk Ahras na alikuwa askofu wa Hippo, ambayo sasa ni mji wa Annaba, kaskazini mashariki mwa Algeria.

Baada ya Algeria, kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki atatembelea Cameroon, Angola na Guinea ya Ikweta.

Leo atakuwa Yaounde, Bamenda na Douala kuanzia Aprili 15 hadi 18; kisha Luanda, Muxima na Saurimo kati ya Aprili 18 na 21; kabla ya kusafiri kwenda Malabo, Mongomo na Bata kati ya Aprili 21 na 23.

Amani na mazungumzo

Papa anatarajiwa kutoa wito wa amani na mazungumzo akiwa Angola na Cameroon, ambako mapambano ya muda mrefu ya kujitenga bado yanaendelea na kusababisha vifo.

Ziara ya mwisho ya papa barani Afrika ilikuwa pale mtangulizi wa Leo, Pope Francis, alipotembelea Jamhuri ya Kideomkarasia ya Congo na Sudan Kusini mwezi Februari 2023.

Kabla ya safari yake ya Afrika, papa atatembelea Monaco kwa siku moja, kwa mujibu wa Vatican. Ziara hiyo katika himaya hiyo ndogo iliyo kwenye pwani ya French Riviera itafanyika Machi 28 na itakuwa safari ya kwanza ya papa katika taifa hilo katika enzi za sasa.

Ziara ya Hispania

Leo pia atatembelea Hispania kuanzia Juni 6 hadi 12.

Atazuru kwanza mji mkuu, Madrid, kisha atasafiri hadi Barcelona ambako atazindua mnara mpya na mrefu zaidi wa Kanisa Kuu la Sagrada Familia, kwa mujibu wa tovuti ya Vatican News.

Ziara hiyo inaadhimisha miaka 100 tangu kifo cha mbunifu wake wa Katalunya, Antoni Gaudi, ambaye alitangazwa kuwa “mheshimiwa” (venerable) na Kanisa Katoliki mwaka 2025 – hatua ya kwanza katika mchakato wa kutangazwa mtakatifu.

Baadaye, Leo atasafiri kwenda Visiwa vya Canary, fungu la visiwa vya Hispania vilivyo pwani ya Afrika Magharibi, eneo muhimu katika njia ya wahamiaji kuelekea Ulaya.