Uturuki inasisitiza kuwa ushirikiano na Somalia ni wa kunufaisha pande zote
Uhusiano wa Uturuki na Somalia umekuwa ukiimarika katika miaka ya hivi karibuni, huku nchi hizo mbili zikitarajiwa kuanza uchimbaji wa mafuta katika pwani ya Somalia mwezi Aprili.
Uturuki imesisitiza tena dhamira yake ya kuendeleza ushirikiano wenye manufaa ya pande zote na Somalia, huku ikikanusha madai kwamba makubaliano yake ya nishati na Somalia yanalenga kunufaisha upande mmoja tu.
“Madai yanayoenezwa kwenye baadhi ya mitandao ya kijamii yanayojaribu kuionyesha Uturuki kama nchi inayotafuta faida za upande mmoja katika sekta ya nishati nchini Somalia—hasa kuhusu uchimbaji wa mafuta—ni upotoshaji wa makusudi na taarifa zisizo za kweli zinazolenga kutia doa ushirikiano wa manufaa ya pamoja kati ya nchi hizo mbili,” Kurugenzi ya Mawasiliano ya Uturuki ilisema katika taarifa iliyotolewa siku ya Alhamisi.
Haya yanajiri wakati meli ya Kituruki ya uchimbaji Çağrı Bey, ikielekea Somalia kwa ajili ya uzalishaji wa kwanza kabisa wa mafuta katika historia ya taifa hilo la Pembe ya Afrika—hatua ambayo imeelezwa na pande zote mbili kuwa ni ya muhimu katika kuimarisha uhusiano wao.
Waziri wa Petroli wa Somalia, Dahir Shire, alisema katika mahojiano na TRT Afrika kuwa uchimbaji huo wa mafuta “ulisubiriwa kwa muda mrefu na ni wa kihistoria kwa watu wa Somalia.”
‘Nchi ndugu’
Uchimbaji huo wa mafuta, unaotarajiwa kuanza katika pwani ya Somalia mwezi Aprili, unafuatia shughuli za utafiti zilizofanywa mwaka jana na meli ya Kituruki ya Oruç Reis, baada ya nchi hizo mbili kusaini makubaliano katika sekta ya mafuta na gesi kama sehemu ya kuimarisha ushirikiano wao katika sekta mbalimbali.
Taarifa hiyo pia iliongeza kuwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Shirika la Mafuta la Uturuki (TPAO) na Mamlaka ya Petroli ya Somalia inaeleza wazi kwamba rasilimali asilia ni mali halali ya watu wa Somalia.
"Uturuki na Somalia zinadumisha uhusiano wao kupitia msingi wa ushirikiano wa pande zote, unaoakisi uhusiano kati ya mataifa mawili huru, yenye urafiki na undugu," Uturuki ilisema.
"Wakati mshikamano huu unaendelea kuimarika katika nyanja mbalimbali, ni muhimu kuepuka kutoa taarifa za upotoshaji na propaganda iliyoundwa kudhoofisha ushirikiano huu," iliongeza.