Katika muendelezo wa sehemu nyingine ya mfululizo wetu unaoangazia vipaji vya riadha Afrika, tunamtambulisha Benjamin Fernandi Ratsim.
Ratsim ana umri wa miaka 19, lakini tayari anashiriki mashindano ya kimataifa ya ngazi ya juu katika mbio za mita 5,000, mita 10,000 na mbio za nyika.
Na hebu tazama takwimu zake.
Mafanikio yake makubwa ya awali yalikuja Novemba 2025, alipokimbia umbali wa kilomita 15 kwa muda wa dakika 41 na sekunde 51 nchini Uholanzi.
Matokeo hayo yaliweka rekodi mpya ya taifa la Tanzania katika mbio za kilomita 15.
Kisha akapanda ngazi hadi kwenye jukwaa kubwa zaidi mwaka 2026, akiiwakilisha Tanzania katika Michezo ya Jumuiya ya Madola jijini Glasgow.
Alikimbia mita 5,000 kwa muda wa dakika 13:49.03 na kushika nafasi ya 17, huku akimaliza mbio za mita 10,000 kwa muda wa dakika 27:59.70 na kushika nafasi ya nane.
Matokeo ya mbio za mita 10,000 ni ya kipekee kwa sababu alikuwa akishindana na baadhi ya wakimbiaji hodari wa mbio ndefu kutoka nchi za Jumuiya ya Madola.
Ripoti za wakati huo zilimtaja kama mmoja wa wanariadha chipukizi wa mbio ndefu nchini Tanzania.
Pia mwaka 2026, alikimbia kilomita 10 kwa muda wa dakika 27 na sekunde 47 katika mashindano ya 'World 10K' jijini Bengaluru, India.
Pia amevunja rekodi ya kukimbia chini ya saa moja katika mbio za nusu marathon, akitumia muda wa dakika 59 na sekunde 58 jijini Ras Al Khaimah.
Shirika la Riadha Duniani (World Athletics) kwa sasa linamtambua miongoni mwa wanariadha bora wa mbio za nyika duniani, likimweka katika nafasi ya 44 duniani kwa upande wa wanaume katika mbio za marathon na barabarani kulingana na rekodi zake za sasa.
Kinachofanya matokeo haya kuwa ya kuvutia zaidi ni umri wake.
Akiwa na umri wa miaka 19 tu, Ratsim tayari anarekodi nyakati zinazomweka miongoni mwa wakimbiaji chipukizi mahiri wa mbio ndefu Afrika Mashariki.
Endelea kufuatilia TRT Afrika Swahili tunapoendelea kuibua vipaji vingine vipya na vya kusisimua vya riadha kutoka barani Afrika.



















