Wake wa viongozi Afrika: Chantal Biya wa Cameroon
Muonekano wa Chantal Biya una sifa ya rangi angavu, vipodozi vya ujasiri, na vito vikubwa vya kuvutia na vyenye thamani.
Chantal Biya, mke wa Rais wa Cameroon anajulikana kwa mtindo wake wa kifahari, haswa nywele zake akipenda sana kuvaa mawigi ya rangi na miundo tofauti ili kuendana na mavazi yake na aina ya tukio analohudhuria.
Muonekano wake una sifa ya rangi angavu, vipodozi vya ujasiri, na vito vikubwa vya kuvutia na vyenye thamani.
Anajulikana kwa mavazi yake maridadi, ikiwa ni pamoja na upendo wake kwa mikoba ya "ma designer” wakubwa.
Katika nchi yake mtindo wake umepewa jina la ‘banane,’ na hutumiwa rasmi katika shughuli mbalimbali.
Biya amekuwa na ushawishi katika kueneza aina ya mitindo mengine ambayo imekuwa ikijulikana kama Chantal Biya.
Chantal Pulchérie Vigouroux alizaliwa Disemba 4 mwaka 1970 na aliolewa na Rais wa Cameroon Paul Biya tangu 1994.
Hii ni baada ya mke wa kwanza, Jeanne Irene Biya kufariki mwaka 1992.
Chantal ana watoto wanne, wawili na Rais Biya na wengine wawili kutoka ndoa yake ya kwanza.
Chantal Biya pia anajihusisha na kazi za kuinua jamii.
Mwaka 1994, Biya alianzisha Wakfu wa Chantal Biya Foundation, ambao unasaidia miradi inayolenga kupunguza umaskini na magonjwa, haswa katika muktadha wa maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Kituo cha 'Mother and Child Centre cha Foundation' kinatoa huduma ya kina ya watoto na elimu ya afya, pamoja na ufuatiliaji wa mara kwa mara kwa watoto waliozaliwa na mama wanaoishi na maambukizi.
Kituo hicho kinakuza utafiti wa matibabu, ikiwa ni pamoja na matibabu na maambukizi ya virusi hivyo.
Bi Biya alikuwa mbele katika uzinduzi wa African Synergies, ambao unalenga kutatua changamoto zinazowakabili wanawake na watoto wanaoishi katika maeneo ya mashambani barani humo.
Anajulikana sana kwa jina la utani na la upendo "Chantou" na anajulikana kujihusisha kwa muziki wa Cameroon huku mara nyingi akicheza kwenye shughuli za umma.