| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
WHO yathibitisha kumalizika kwa mlipuko wa Ebola nchini Uganda
WHO iliendelea kufuatilia hali nchini Uganda hadi wiki hii ili kuhakikisha kuwa hakuna athari yoyote ya maambukizi iliokuwa imeachwa bila ya kushughulikiwa.
WHO yathibitisha kumalizika kwa mlipuko wa Ebola nchini Uganda
Hatua ya kutangazwa kuwa Uganda iko salama inafuatia tangazo la serikali ya Uganda la tarehe 28 Julai. / / Reuters

Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha kumalizika kwa mlipuko wa Ebola nchini Uganda. Hata hivyo, ugonjwa huo bado haujadhibitiwa katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mlipuko wa aina ya Bundibugyo ya virusi vya Ebola nchini Uganda umetangazwa kuwa umemalizika, huku hali ikiwa tofauti katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako maambukizi bado yanaendelea kuongezeka. Afisa wa WHO alisema hayo katika mkutano wa Jumatano.

WHO iliendelea kufuatilia hali nchini Uganda hadi wiki hii ili kuhakikisha kuwa hakuna athari yoyote ya maambukizi iliokuwa imeachwa bila ya kushughulikiwa.

Tangazo hilo la WHO linafuatia taarifa ya Serikali ya Uganda ya Julai 28 kwamba mlipiko wa Ebola umemalizika nchini humo. Mlipuko huo ulisababisha jumla ya maambukizi 20 na vifo viwili nchini humo.

Maambukizi bado yanaendelea DRC

Kwa upande wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Dk. Marie Roseline Belizaire, mkurugenzi wa maandalizi ya dharura wa WHO katika kanda ya Afrika, alisema idadi ya maambukizi bado inaongezeka licha ya hatua kadhaa za kudhibiti mlipuko huo.

Mlipuko huo nchini DRC ni miongoni mwa milipuko mabaya zaidi ya Ebola kuwahi kutokea, ukiwa wa pili kwa kusababisha vifo vingi katika historia ya ugonjwa huo na kwa sasa ukiendelea kwa kasi zaidi kuliko juhudi za kuudhibiti.

Kwa mujibu wa Serikali ya Congo, hadi Jumanne kulikuwa na zaidi ya vifo 2,700 na zaidi ya maambukizi 5,600 vya Ebola.

“Maambukizi bado yanaendelea kwa kiwango kikubwa,” alisema Belizaire. “Tumepunguza kasi ya ongezeko, lakini bado hatujaweza kubadili mwelekeo wa hali hii.”

Alisema kuna maboresho katika ufuatiliaji wa watu walioambukizwa na wagonjwa pamoja na upimaji wa ugonjwa huo. Pia alisema uchambuzi wa virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo haujaonyesha dalili zozote za mabadiliko ya kijenetiki, licha ya ugonjwa huo kuenea kwa kasi.

Ingawa alieleza kuwa kutokuwepo kwa mabadiliko hayo ni habari njema, Belizaire alionya kuhusu upungufu wa Dola milioni 30 za Marekani unaohitajika kugharamia shughuli za usafirishaji na ugavi wa vifaa vya matibabu pamoja na vifaa vya kujikinga kwa wahudumu wa afya katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi nchini Congo.

“Bila uwekezaji huu wa haraka, tunahatarisha kusitisha kasi ya maendeleo ambayo tumeijenga,” alisema.

CHANZO:Reuters