Kwa nini nchi huamua kuhamisha mji wake mkuu?
Bunge la Taifa la Tanzania lipo Dodoma , mji mpya mkuu wa nchi hiyo ikiwa Tanzania ilihamisha rasmi makao yake makuu kutoka Dar es Salaam / Reuters
Kwa nini nchi huamua kuhamisha mji wake mkuu?
Miji mikuu mingi ilitengwa na wakoloni, hivyo kwa nchi nyingi kuchagua mji mpya ni kama mwanzo mpya na njia ya kukaa mbali na historia ya ukoloni.
10 Machi 2026

Miji mikuu mingi katika nchi za Kiafrika ilitengwa wakati wa ukoloni lakini baadhi ya nchi baadae ziliamua kuhamisha miji mikuu na kuipeleka sehemu nyengine.

Kwa mfano, Nigeria ilihamisha mji mkuu wa pwani wa Lagos hadi mji wa katikati wa Abuja mnamo 1991.

Tanzania ilihamisha rasmi makao yake makuu kutoka Dar es Salaam hadi katikati mwa jiji la Dodoma, na mchakato huo ukakamilika kwa kiasi kikubwa mwaka 2019.

Côte d'Ivoire ilihamisha mji wake mkuu wa kisiasa kutoka Abidjan hadi jiji la Yamoussoukro mwaka 1983, ingawa majukumu mengi ya kiutawala yalisalia Abidjan.

Burundi ilihamisha mji mkuu wa kisiasa kutoka Bujumbura hadi Gitega mnamo 2018 ili kukuza maendeleo ya kikanda, wakati Bujumbura ikisalia kuwa kitovu cha uchumi.

Equitorial Guinea  ilihamisha mji mkuu kutoka mji wa kisiwa cha Malabo hadi bara, haswa mji mpya uliojengwa wa Ciudad de la Paz ambao zamani ulijulikana kama Oyala.

Malawi ilihamisha mji wake mkuu kutoka Zomba hadi Lilongwe mwaka 1975.

Botswana nayo ilihamisha mji wake mkuu kutoka Mafikeng iliyoko Afrika Kusini hadi Gaborone baada ya kupata uhuru katika miaka ya 1960.

Mauritania mnamo 1958 ilichagua Nouakchott kama mji mkuu ikichukua nafasi ya Saint-Louis ambayo kwa sasa iko katika Senegal- ambayo ilitumika kama kituo cha utawala cha koloni la Ufaransa.

Lakini kwa nini nchi zilihamisha miji yao mikuu?

Kwa sababu miji mikuu mingi ilitengwa na wakoloni, hivyo kwa nchi nyingi kuchagua mji mpya ni kama mwanzo mpya na njia ya kukaa mbali na historia ya ukoloni.

Pia inasaidia kuepukana na changamoto ya kulemewa na idadi ya watu na hapo kuathiri miundo mbinu muhimu kama mifereji ya maji ambayo huweza kusababisha mafuriko, kuhimiza usafi na kuhakikisha ujenzi unafanywa kwa mpangilio.

Mabadiliko ya eneo pia husaidia kupunguza msongamano unaosababishwa na ongezeko la watu.

Miji mikuu ya pwani kwa mfano mara nyingi ilianzishwa wakati wa ukoloni kama Lagos na Dar es Salaam na kwa muda idadi ya watu iliongezeka, na hapo kufanya upanuzi kuwa mgumu.

Nchi kuamua kuhamisha mji mkuu kwenda eneo jengine lisiloegemea upande wowote kisiasa au kikabila pia husaidia kuunganisha makabila mbalimbali na kuleta serikali karibu na wancnhi wake.

Uhamisho hutumiwa kuchochea ukuaji katika maeneo duni ya ndani au vijijini.

Miji barani Afrika inayotambulika kuwa na mipango mizuri ni pamoja na Abuja nchini Nigeria, Kigali nchini Rwanda, Addis Ababa nchini Ethiopia na Gaborone, nchini Botswana.

Rabat nchini Morocco, Port Lous nchini Mauritius na Lilongwe nchini Malawi pia zinasifika kwa kuwa na mpangilio mwema unaonedana na idadi ya wananchi wake.

CHANZO:TRT Swahili