Natasha Museveni: Binti wa kwanza wa Rais wa Uganda mwenye nafasi ya kipekee
Mmoja wa watu maarufu ambae anavutia wengi nchini Uganda ni Natasha Museveni Karugire/ Picha kutoka @NyinancweendeX / Public domain
Natasha Museveni: Binti wa kwanza wa Rais wa Uganda mwenye nafasi ya kipekee
Natasha Museveni hana nafasi serikalini, lakini amekuwa machoni mwa watu kutokana na nafasi yake katika mitindo na filamu huku akisaidia uongozi wa baba yake.
21 Machi 2026

Mmoja wa watu maarufu ambae anavutia wengi nchini Uganda ni Natasha Museveni Karugire.

Ni binti mkubwa wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni na mara nyingi anaonekana akiwa pamoja na baba yake katika shughuli za umma.

Natasha hana nafasi rasmi katika serikali ya Uganda, lakini ameweza kujenga taswira ya umma kupitia kazi zake katika mitindo, filamu na utamaduni, huku akisaidia serikali ya baba yake.

Kazi ya ubunifu ya Natasha mara nyingi inajikita katika kuangalia historia ya familia yake na urithi wa Uganda na utamaduni.

Hii inamuweka katika nafasi ya kipekee ambayo inajumuisha ubunifu wa ujasiriamali na ushawishi wa kisiasa.

Alama ya mitindo

Mwaka 2003, alizindua alama ya mtindo, House of Karugire, ambayo baadae iligeuka na kuwa J & Kainembabazi, baada ya kujifunza mitindo na masoko katika Chuo Kikuu cha American Intercontinental University mjini London.

Kama mtengezaji filamu , aliongoza filamu yake ya kwanza ya mwaka 2018 '27 Guns' – tamthilia ya wasifu inayoonesha hatua za Mapigano ya Msitumi katika miaka ya 80, ikijikita kuonesha mchango wa baba yake katika mapambano, ambayo yalimuingiza madarakani mwaka 1986.

Mwaka 2020, Natasha aliandika kumbukumbu, na baadae kuanzisha podcast mwaka 2023 kuhusu mada za utamaduni wa Kiafrika.

Natasha alizaliwa katika nchi jirani ya Tanzania Machi, 1976, ambapo baba yake alikuwa akiishi uhamishoni.

Mwaka 2024 katika mahojiano ya kuadhimisha miaka 80 ya kuzaliwa kwa baba yake, Natasha alisimulia kumbukumbu ya familia yake ya kuishi uhamishoni, ikiwemo Kenya na Sweden.

Anasimulia jinsi, wakati mmoja, alivyoshindwa kumtambua baba yake pindi alipowatembea nchini Sweden.

Mazoezi ya jeshi

Natasha pia alizungumzia kuhusu ratiba kali ya baba yake, ikiwemo kuwaamsha mapema alfajiri kufanya mazoezi.

Licha ya ukali wa Museveni, Natasha anasema amekuwa muelewa na kumuunga mkono katika kazi zake.

Katika miaka ya hivi karibuni, Natasha mara nyingi amekuwa akimsindikiza baba yake katika shughuli mbalimbali za kisiasa.

Hata hivyo, mwishoni mwa kwaka 2025, alipoulizwa katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu uwezekano wa Natasha au dada zake kuingia katika siasa, Rais Museveni alisema: "Hawezi kuingia katika siasa na kuanza kupigania hizi kazi."

Wakati Museveni akiondoa uwezekano wa binti zake kuingia katika siasa za taifa, kijana wake wa pekee, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, hivi sasa ndie Mkuu wa Majeshi wa Uganda na siku za nyuma ameonesha nia ya kumrithi baba yake kama rais wa Uganda.

CHANZO:TRT Afrika