Mwanajeshi wa zamani wa Uingereza anayesakwa nchini Kenya kwa mauaji anyimwa dhamana
Mwili wa Wanjiru ulipatikana kwenye tanki la maji taka katika Hoteli ya Lion's Court katika mji wa Nanyuki nchini Kenya mnamo Juni 2012. Wanjir alionekana mara ya mwisho akiwa na kundi la wanajeshi wa Uingereza usiku wa Machi 31 na Aprili 1, 2012.
Mwanajeshi wa zamani wa Uingereza anayesakwa nchini Kenya kutokana na mauaji ya mwanamke karibu na kambi ya mafunzo ya jeshi la Uingereza miaka kumi na mbili iliyopita alinyimwa dhamana siku ya Jumatatu akisubiri kesi ya kurejeshwa nchini humo.
Robert Purkiss anatuhumiwa kumuua Agnes Wanjiru mwenye umri wa miaka 21 karibu na kambi ya mafunzo ya jeshi mwaka 2012, huku mamlaka ya Kenya ikitoa hati ya kukamatwa kwake mwezi Septemba.
Purkiss, ambaye alikamatwa mwezi huu na amekuwa kizuizini tangu, "anakanusha vikali" kuhusika na kifo cha Wanjiru, mawakili wake waliambia Mahakama ya Westminster.
Mawakili wanaowakilisha mamlaka nchini Kenya wanasema wanajeshi wenzake Purkiss wanadai kuwa alikiri kufanya mauai hayo usiku wa tukio.
Mauaji ya Wanjiru yamezorotesha uhusiano kati ya Uingereza na Kenya, ambapo familia yake na mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema wauaji walikuwa wakilindwa na makubaliano ya ushirikiano wa kiulinzi ambayo yanatatiza kufunguliwa mashtaka kwa wanajeshi wa Uingereza waliokuwa wakifunzwa nchini Kenya.
Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema mnamo Septemba iliendelea kujitolea kusaidia familia ya Wanjiru kupata haki.
Mwili wa Wanjiru ulipatikana kwenye tanki la maji taka katika Hoteli ya Lion's Court katika mji wa Nanyuki nchini Kenya mnamo Juni 2012. Wanjir alionekana mara ya mwisho akiwa na kundi la wanajeshi wa Uingereza usiku wa Machi 31 na Aprili 1, 2012.