Arsenal kusitisha ushirikiano wake na Visit Rwanda
Baada ya miaka nane ya nembo ya Visit Rwanda kupamba bega la jezi za Arsenal, klabu hiyo ilitangaza kuwa itasitisha mkataba wa udhamini na Visit Rwanda ifikapo mwezi Juni 2026.
Hata hivyo, ushirikiano huu haukupita bila changamoto. Makundi ya haki za binadamu yalieleza wasiwasi kuhusu kuhusishwa kwa serikali ya Rwanda na kundi la M23 linalopigana dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa madai. Madai ambayo Rwanda inaendelea kuyakataa.
Haya yanajiri baada ya kundi la M23 na serikali ya DRC kukubali kusitisha mapigano mapema wiki hii.
Licha ya shinikizo hizi, pande zote mbili zilikanusha kuwa sababu za kisiasa ndizo zilizopelekea kusitishwa kwa mkataba.
Katika taarifa, Arsenal ilikiri mchango mkubwa wa ushirikiano huo. Msemaji wa klabu alisema, “Uhusiano wetu na Visit Rwanda umekuwa sehemu muhimu ya mkakati wetu wa kibiashara kimataifa. Tumefanikiwa kufanya mambo makubwa pamoja, kuanzia programu za kijamii hadi kuongezea mwonekano wa Rwanda duniani.”
Kwa upande wa Rwanda, mafanikio ya ushirikiano huo yalisisitizwa pia. Mwakilishi wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda alisema, “Tulipoanza safari hii, lengo letu lilikuwa kuutambulisha utalii wa Rwanda kwa dunia. Kilichopatikana katika ushirikiano huu, ongezeko la watalii, kutambulika kimataifa, na ushirikiano wa kitamaduni — kilizidi matarajio yetu. Tunashukuru Arsenal kwa miaka nane yenye mafanikio.”