Rais wa Israel akutana na kiongozi wa eneo lililojitenga la Somaliland mjini Davos

Kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya pande hizo mbili kumekosolewa vikali kote duniani kwa kukiuka uhuru wa Somalia.

By
Wawili hao walikutana kando ya Kongamano la Kiuchumi la Dunia mjini Davos, Uswizi. / Wengine / Others

Rais wa Israel, Isaac Herzog, siku ya  Alhamisi alikutana na kiongozi wa eneo la Somaliland lililojitenga na Somalia pembeni mwa mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum) uliofanyika Davos, Uswizi.

Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X Herzog alisema alikuwa “na furaha” kukutana na rais aliyejitangaza wa Somaliland, Abdirahman Mohamed Abdullahi, wakati wa mkutano huo wa kila mwaka.

Alisema anapongeza kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya pande hizo mbili na akaeleza matumaini ya kupanua ushirikiano wa pande mbili “kwa manufaa ya watu wa mataifa yote mawili.”

Mnamo Disemba 26, Israel ilitangaza kuwa imetambua rasmi Somaliland kama taifa huru na lenye mamlaka kamili, na hivyo kuwa nchi pekee duniani kufanya hivyo. Hatua hiyo ilikosolewa vikali kote duniani.

Somalia ilithibitisha tena msimamo wake thabiti na usiokuwa na mjadala wa kulinda mamlaka yake, umoja wa kitaifa, na uhuru wa mipaka yake, na ikaikataa hatua ya Israel.

Somaliland imekuwa ikijiendesha kama eneo linalojitawala tangu ilipotangaza kujitenga na Somalia mwaka 1991, lakini haijapata kutambuliwa kimataifa kama taifa huru.

Kutambuliwa kwa Somaliland na Israel kunakiuka sheria za kimataifa na kunaakisi ushindani wa kupata ushawishi katika Ghuba ya Aden, mojawapo ya njia muhimu za usafiri wa baharini duniani, inayorahisisha takribani asilimia 15 ya biashara ya kimataifa.