| Swahili
UTURUKI
3 dk kusoma
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Fidan kufanya ziara rasmi ya siku mbili nchini Uingereza
Waziri wa Mambo ya Nje Hakan Fidan anatarajiwa kujadili masuala ya biashara, ushirikiano wa kijeshi, usalama wa kikanda na changamoto za ukazi zinazoathiri raia wa Uturuki wakati wa ziara yake.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Fidan kufanya ziara rasmi ya siku mbili nchini Uingereza
Hakan Fidan akijibu maswali wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Antalya, Uturuki, Aprili 19, 2026. / AA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, anatarajiwa kufanya ziara rasmi ya siku mbili nchini Uingereza kuanzia Alhamisi, ambapo atafanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Yvette Cooper, wabunge wa Uingereza na maafisa wengine wa serikali, kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia.

Wakati wa ziara yake London, Fidan pia anatarajiwa kuhutubia katika hafla itakayofanyika katika Kituo cha Historia ya Dunia cha Chuo Kikuu cha Oxford pamoja na Progamu ya Mpangilio wa Dunia (Global Order Program), na kukutana na jamii ya Kituruki pamoja na wawakilishi wa biashara wanaoishi Uingereza.

Vyanzo hivyo vimesema Fidan anatarajiwa kueleza kuridhishwa kwake na mwenendo chanya wa uhusiano kati ya Uturuki na Uingereza, na kujadili juhudi za pamoja za kupanua ushirikiano uliopo na kuimarisha uhusiano kwa njia pana zaidi.

Pia anatarajiwa kusisitiza umuhimu wa kukamilisha mazungumzo ya kuboresha Mkataba wa Biashara Huria uliopo ili kuongeza kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili.

Fidan anatarajiwa kusisitiza kuwa jamii ya Waturuki takribani 500,000 wanaoishi Uingereza ni sehemu muhimu sana inayochangia kuimarisha uhusiano wa kibinadamu, kitamaduni na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.

Vyanzo vya kidiplomasia vinasema waziri huyo wa mambo ya nje huenda akazungumzia pia ucheleweshaji wa maombi ya ukazi ya kudumu kwa raia wa Uturuki na kueleza matarajio ya hatua za haraka kushughulikia suala hilo.

Mazungumzo hayo pia yanatarajiwa kuangazia azma thabiti ya kisiasa ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya ulinzi na kukuza ushirikiano katika sekta ya nishati, ikiwemo nishati ya nyuklia na nishati mbadala.

Uingereza ni soko la pili kwa ukubwa la mauzo ya nje ya Uturuki

Katika mazungumzo hayo, Fidan atasisitiza umuhimu wa mipango ya usalama na ulinzi ya Umoja wa Ulaya kufanyika kwa uratibu wa karibu na NATO, kwa mujibu wa vyanzo hivyo.

Maendeleo ya kikanda pia yanatarajiwa kujadiliwa kwa kina, ikiwemo mazungumzo yanayoendelea kati ya Iran na Marekani yanayoendeshwa na Pakistan, hali ya Mlango-Bahari wa Hormuz, pamoja na juhudi za kidiplomasia kumaliza vita vya Urusi na Ukraine kwa amani ya haki na endelevu.

Fidan pia anatarajiwa kusisitiza haja ya msimamo wa kimataifa ulio na kanuni, mshikamano na uamuzi dhidi ya hatua za Israel zinazodhoofisha usitishaji mapigano Gaza na suluhisho la mataifa mawili, pamoja na umuhimu wa kuweka hali ya kibinadamu ya Palestina katika ajenda ya kimataifa. Pia atasisitiza umuhimu wa kuunga mkono mipango inayolenga utulivu wa muda mrefu na ujenzi upya wa Syria.

Ziara hii inafuatia mawasiliano ya hivi karibuni ya ngazi ya juu kati ya nchi hizo mbili.

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer alitembelea Uturuki mnamo 27 Oktoba 2025, ambapo alikutana na Rais Recep Tayyip Erdogan, na makubaliano yakasainiwa kukamilisha ununuzi wa ndege za kivita za Eurofighter Typhoon kwa Uturuki.

Fidan alifanya ziara yake ya mwisho London tarehe 30 Oktoba 2024, na pia alihudhuria mkutano kuhusu Ukraine ulioandaliwa na Uingereza London Machi 2–3 mwaka uliopita. Pia alikutana na Cooper pembezoni mwa Jukwaa la Diplomasia la Antalya Jumamosi iliyopita.

Uingereza bado ni mmoja wa washirika wakuu wa biashara wa Uturuki. Kiwango cha biashara kati ya nchi hizo kilifikia dola bilioni 26 mwaka 2025, huku pande zote zikilenga kukifikisha dola bilioni 30, kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia.

Uingereza ilikuja kuwa soko la pili kwa ukubwa la mauzo ya nje ya Uturuki mwaka 2025, na ilibaki miongoni mwa nchi tatu za juu kwa uwekezaji wa kigeni na utalii. Kati ya 2002 na 2025, uwekezaji wa Waingereza nchini Uturuki ulifikia dola bilioni 14.5, huku uwekezaji wa Waturuki nchini Uingereza ukifikia dola bilioni 3.5. Mwaka 2025, watalii milioni 4.3 kutoka Uingereza walitembelea Uturuki.

Mazungumzo ya kupanua wigo wa Mkataba wa Biashara Huria kati ya nchi hizo mbili yanaendelea, huku yakilenga kukamilika mwaka 2026, kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia.

CHANZO:AA