Bondia Anthony Joshua aruhusiwa kutoka hospitali

Imethibitishwa kwamba, afya ya bingwa wa zamani wa ngumi za uzito wa juu iko imara, kuruhusiwa kutoka hospitali na kufuatilia maendeleo ya afya yake akiwa nyumbani.

By
Anthony Joshua arrives for the heavyweight boxing match against Jake Paul. / AP

Bingwa wa zamani wa ngumi za uzito wa juu duniani, Anthony Joshua, ameruhusiwa kutoka hospitali, hii ni kwa mujibu wa maafisa wa serikali nchini Nigeria. Joshua alisalimika katika ajali ya gari iliyoua marafiki zake wawili wa karibu.

Bondia huyo kutoka nchini Uingereza, alikuwa safarini nchini Nigeria alipopata ajali siku ya Jumatatu akiwa pamoja na marafiki Sina Ghami na Latif Ayodele.

Ajali hiyo ilitokea katika barabara kuu inayounganisha jiji la Lagos na Ibadan kusini-magharibi mwa nchi.

Uchunguzi wa awali unaonesha gari waliyokuwa wakisafiria ilipasuka tairi ikiwa katika mwendo wa kasi, haya ni kwa mujibu wa Wakala wa Polisi wa Usalama Barabarani (TRACE) katika jimbo la Ogun.

"Anthony Joshua ameruhusiwa kutoka hospitali, ili afuatilie maendeleo ya afya yake akiwa nyumbani" ilisema taarifa ya pamoja iliyotolewa na wazungumzaji wa serikali za jimbo la Lagos na Ogun.

"Ingawa amejawa na huzuni baada ya kupoteza marafiki zake wawili wa karibu, alifanyiwa uchunguzi wa kiafya na kubainika kuwa anaweza kurudi nyumbani," alisema msemaji wa jimbo la Lagos Gbenga Omotoso na mwenzake wa Ogun Kayode Akinmade.

Serikali za majimbo yote mawili zimekuwa zikisimamia matibabu ya Joshua tangu ajali ilipotokea Jumatatu.

Baada ya kutoka hospitali, Joshua na mama yake walikwenda kuangalia miili ya marafiki zake 'iliyokuwa ikiandaliwa kwa ajili ya kurejeshwa nyumbani,' ilisema taarifa.

Polisi nchini Nigeria ilisema waathiriwa wawili hao walikufa hapo hapo baada ya ajali.