Nigeria sasa imejiunga na nchi chache za Kiafrika, ikiwa ni pamoja na Kenya na Ghana, katika kupata idhini zaidi ya viza kwa wataalamu wao wanaotafuta kazi nchini Marekani.
Viza za kazi kwa hadi 60% ya Wanigeria viliidhinishwa na Marekani katika siku za hivi majuzi, na hivyo kubadilisha muundo wa awali wa viwango vya juu vya kukataliwa.
Travel and Tour World, jukwaa ambalo huandika matukio yanayohusiana na uhamiaji, inaripoti kwamba katika kazi zenye mishahara mikubwa, kiwango cha kuidhinisha viza kwa Wanigeria kilikuwa cha juu kama 75%.
Hii inaonyesha nia ya Marekani kuendelea kuwachukua watu binafsi au watendaji wenye ujuzi wa hali ya juu, hasa kutoka Afrika.
Ada ya viza za kazi ya $100,000
Wakati kiwango cha uidhinishaji wa viza kwa Wanigeria wanaotafuta kazi nchini Marekani kimeongezeka, rekodi zinaonyesha kuwa makampuni machache ya Marekani yalikuwa tayari kutenga $100,000 kwa kila mfanyakazi wa kigeni.
Ada hii, ya upatikanaji wa talanta kutoka nje, ilianzishwa na Rais Donald Trump mnamo Septemba 2025, na italipwa na kampuni ya inayoajiri.
Kwa sababu ya kuongezeka kwa gharama hii, Travel and Tour World inaripoti kwamba kumekuwa na kushuka kwa 43% kwa maombi ya viza ya kazi kwa raia wa kigeni.
Raia wa Nigeria, ambao tayari walikuwa wameajiriwa na makampuni ya Marekani wakati ada ya viza ya kazi ilipowekwa Septemba mwaka jana, wameondolewa kwenye malipo hayo.
Hofu ya kupoteza wataalamu
Hii inazifanya zivutie sana kampuni za Marekani, haswa zile za sayansi na kiufundi.
Huku zaidi ya Wanigeria 300,000 wanaofanya kazi Marekani, taifa hilo la Afrika Magharibi lina idadi kubwa zaidi ya Waafrika wanaofanya kazi Marekani.
Ingawa kufyonzwa kwa Wanigeria katika soko la Marekani kunaweza kuashiria kuongezeka kwa imani katika ujuzi wao, wasiwasi umeibuliwa nyumbani kwamba unachangia kudhoofisha ubongo, na kuwaacha wafanyakazi wa nyumbani kukosa ujuzi muhimu katika sayansi na teknolojia.
Travel and Tour World inakadiria kuwa uhaba wa wataalamu wenye ujuzi wa juu nchini Nigeria unaweza kuongezeka kwa hadi 20% katika miaka ijayo.
Wakenya, Waghaana pia wanatafutwa sana
Ghana, Misri, Kenya, Afrika Kusini, Ethiopia, na Zimbabwe pia zimeona ongezeko la idadi ya raia wao kuajiriwa katika soko la ajira la Marekani miaka ya hivi karibuni.
Viwango vya idhini ya viza za kazi kwa raia wa nchi hizi viko juu sana ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika.
Kampuni zinazochukua wahitimu Wakenya ambao tayari wako Marekani, kwa mfano, hulipa tu $215 kwa viza zao za kazi, badala ya $100,000, jambo linalowafanya Wakenya kuwa faida kwa kampuni za Marekani.
Uhandisi, usanifu, Teknolojia ya Habari, na utafiti ni nyanja kuu ambazo Marekani inatafuta kujaza kwa kutumia talanta kutoka nje.
“Kazi maalum”
Wahamiaji wa kigeni wanaofanya kazi kwa kampuni za Marekani wanapangiwa viza ya H-1B.
Hii ni viza ya wasiohamiaji inayounga mkono mwajiri na kuruhusu kampuni za Marekani kuajiri wataalamu wa kigeni katika "kazi maalum" zinazohitaji ujuzi maalum sana na angalau shahada ya kwanza.
Kabla Rais Trump hajoinua gharama ya maombi ya viza ya H-1B hadi $100,000, iligharimu, kwa wastani, takriban $5,000 kwa kila mtu.

















