Chama cha Wanasheria nchini Kenya (LSK) kimetangaza kususia huduma za mahakama kote nchini Jumatano, Julai 22, 2026, kupinga kile kinachokitaja kuwa ni kushindwa katika uendeshaji wa haki na kushinikiza kufanyika kwa mageuzi ya taasisi.
Rais wa LSK, Charles Kanjama, alisema mgomo huo wa siku moja utawataka mawakili kujiondoa katika kushiriki kwenye vikao vyote vya mahakama pamoja na maombi yanayowasilishwa mahakamani.
LSK imetoa orodha ya majaji watakaoathiriwa na ususiaji huo wa kitaifa unaoanza Jumatano, Julai 22, huku mawakili wakiongeza shinikizo la kutaka mageuzi yafanywe katika Idara ya Mahakama.
Miongoni mwa waliotajwa kwenye orodha hiyo ni Jaji Mkuu Martha Koome, Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu, pamoja na majaji wa Mahakama ya Juu Isaac Lenaola, Smokin Wanjala na Njoki Ndung’u.
Akizungumza mjini Machakos baada ya kukutana na viongozi wa Tawi la Kusini Mashariki na Kitengo cha Machakos, Kanjama alifafanua kuwa ususiaji huo hautahusisha uwasilishaji wa kesi mpya mahakamani.
Masuala yaliyoibuliwa na mawakili yanahusu uendeshaji wa shughuli za sajili za mahakama, usimamizi wa mahakama, uwajibikaji wa majaji, heshima ya taaluma ya sheria, pamoja na mazingira ya kazi kwa mawakili.
“...Mawakili wanaendelea kukumbwa na ucheleweshaji wa kusikilizwa na kutolewa maamuzi ya kesi, pamoja na kucheleweshwa kwa utoaji wa hukumu. Wanachama wameripoti kuwepo kwa uzembe unaoendelea katika sajili za mahakama na wameeleza wasiwasi kuhusu ufanisi wa mifumo ya kushughulikia malalamiko dhidi ya majaji na maafisa wa mahakama,” alisema Kanjama.
“Kwa kuzingatia changamoto hizi, Baraza limeamua kufanya ususiaji wa shughuli za mahakama kote nchini Jumatano, Julai 22, 2026. Ususiaji huo unalenga kuonyesha uzito wa masuala yaliyoibuliwa na wanachama na kutoa wito wa kuwepo kwa hatua za maana za kitaasisi zitakazorejesha imani katika usimamizi wa haki.”











