Wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF) nchini Sudan wameshambulia msafara wa misaada wa Umoja wa Mataifa katika jimbo la Kordofan Kusini, na kusababisha kifo cha mtu moja na wawili kujeruhiwa, kundi la madaktari la eneo hilo lilisema siku ya Alhamisi.
Katika taarifa, Mtandao wa Madaktari wa Sudan unasema kuwa msafara huo ulishambuliwa katika mji wa Dilling wakati ukiwa njiani kuelekea Kadugli, mji mkuu wa Kordofan Kusini.
Mtu mmoja aliuawa na madereva wawili wa malori walijeruhiwa katika mashambulizi hayo, kundi hilo lilisema.
Linasema kuwa msafara ulikuwa umebeba misaada ya watu zaidi ya 5,000 wanaokabiliwa na uhaba wa chakula, dawa na bidhaa za msingi.
Kundi hili lilishtumu mashambulizi hayo, likiyataja kuwa mtindo wa mashambulizi ya RSF unaojirudia hasa kwa misafara ya misaada na raia.
Linasema kuwa kushambulia misaada na kuzuia operesheni za misaada ni ukiukwaji wa sheria ya kimataifa.
Kundi hilo limetoa wito kwa jamii ya kimataifa, Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada kuhakikisha usalama, na ufikishaji wa misaada kwa raia kote nchini Sudan bila pingamizi.
Pia lilitaka uongozi wa RSF kusitisha mashambulizi kwa misafara ya misaada na wafanyakazi wake na kuwataka wale waliohusika kuwajibishwa.
Wiki iliopita, Umoja wa Mataifa ulisema kuwa raia 1,100 waliuawa kwa mashambulizi ya droni kote nchini Sudan kati ya Januari na Juni mwaka huu.


















