Tathmini za siri za kijasusi za Marekani zinaonyesha kuwa Iran bado ina uwezo mkubwa wa kurusha makombora, kulingana na ripoti ya vyombo vya habari vya Marekani.
Gazeti la The New York Times liliripoti kwamba taarifa za kijasusi za mapema mwezi Mei zinaonyesha Iran imerejesha uwezo wa kiutendaji katika sehemu nyingi za makombora yake, ikiwemo maeneo 30 kati ya 33 yaliyo karibu na Mlango-Bahari wa Hormuz.
Likilinukuu watu wanaofahamu tathmini hizo, gazeti hilo lilisema Iran bado inamiliki takriban asilimia 70 ya akiba yake ya makombora ya kabla ya vita pamoja na vifaa vya kurushia makombora vinavyohamishika.
Tathmini hizo pia ziligundua kuwa karibu asilimia 90 ya vituo vya chini ya ardhi vya kuhifadhi na kurushia makombora kote nchini Iran sasa “vinafanya kazi kwa kiwango fulani au kikamilifu.”
Hata hivyo mara kwa mara Rais wa Marekani Donald amekuwa akijigamba kuwa Marekani "imeharibu kabisa uwezo wa kijeshi wa Iran".
Msemaji wa White House akana kuimarishwa tena kwa jeshi la Iran
Msemaji wa Ikulu ya White House, Olivia Wales, alinukuliwa akisema kuwa serikali ya Iran inajua kwamba “hali yake ya sasa si endelevu” na kwamba yeyote “anayefikiri Iran imejenga upya jeshi lake huenda akawa amepoteza mwelekeo au ni msemaji wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu cha Iran (IRGC).”
Mvutano wa kikanda umeongezeka tangu Marekani na Israel zilipoanzisha mashambulizi dhidi ya Iran mnamo Februari 28, jambo lililosababisha Iran kujibu kwa mashambulizi dhidi ya Israel pamoja na washirika wa Marekani katika Ghuba, sambamba na kufungwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz.
Makubaliano ya kusitisha mapigano kwa wiki mbili yalianza kutekelezwa Aprili 8 kupitia upatanishi wa Pakistan, lakini mazungumzo yaliyofuata mjini Islamabad hayakufanikiwa kufikia makubaliano ya kudumu.
Baadaye, Trump aliongeza muda wa usitishaji huo wa mapigano kwa kipindi kisicho na kikomo. Tangu wakati huo, Islamabad imekuwa ikijaribu kufufua diplomasia iliyokwama.
Trump alikataa jibu la hivi karibuni la Iran kuhusu pendekezo la Marekani la kumaliza vita kabisa, akiliita kuwa “halikubaliki kabisa.”















