Sudan yalaani 'shambulizi la kikatili' la RSF katika hospitali wakati wa utoaji chanjo kwa watoto
Wizara ya Mambo ya Nje imesema shambulizi hilo limefanyika katika Hospitali ya Al-Jabalain katika jimbo la White Nile wakati wa kampeni ya chanjo kwa watoto.
Sudan imelaani vikali shambulizi lililofanywa na vikosi vya RSF katika Hospitali ya Al-Jabalain katika jimbo la White Nile, na kulitaja kama "uhalifu wa kikatili."
Watu saba wameuawa, wakiwemo watumishi wawili wa afya, huku 11 wengine wakijeruhiwa katika shambulizi hilo la anga lililotokea siku ya Alhamisi.
Al-Jabalain ni hospitali pekee iliyopo katika eneo hilo, kwa mujibu wa Mtandao wa Madaktari Sudan.
Mtandao huo unasema shambulizi hilo limeharibu sehemu za jengo pamoja na vifaa tiba.
Katika taarifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan imesema shambulizi hilo limefanyika wakati wa kampeni ya kutoa chanjo kwa watoto, na kusema huo ni ushahidi zaidi unaolenga raia na miundombinu ya afya.
Kutatiza huduma muhimu
Wizara pia ilisema RSF wamelenga eneo la hifadhi ya madawa na vituo vya mafuta katika mji wa Rabak kama moja wapo ya jitihada za kutatiza huduma kwa wananchi.
Sudan imeutaka Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani shambulizi hilo na kuchukua hatua za haraka kusitisha ukiukaji wa sheria na kuwawajibisha wahusika.
Mpaka sasa RSF haijasema lolote kuhusiana na tuhuma hizo.
Katika majimbo 18 ya Sudan, RSF inadhibiti majimbo yote matano katika mkoa wa magharibi mwa Darfur isipokuwa sehemu ya Kaskazini mwa Darfur, ambayo inabaki
chini ya udhibiti wa jeshi.
Jeshi linadhibiti sehemu kubwa ya majimbo 13 yaliyobaki kusini, kaskazini, mashariki na kati ya nchi, ikiwemo mji mkuu wa Khartoum.
Mgogoro kati ya jeshi la Sudan na RSF, ulianza Aprili 2023, na mpaka sasa maelfu wamepoteza maisha, huku mamilioni wakikosa makazi.