Waziri Mkuu wa Tanzania Mwigulu Nchemba amewahimiza viongozi na watendaji wa Serikali kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha usalama wa kikanda ili kuchochea uwekezaji wa kikanda na kimataifa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo Alhamisi, Aprili 16, 2026 mkoani Kigoma wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji la Ziwa Tanganyika, linalofanyika kwa siku nne mjini Kigoma.
Kongamano hilo ambalo linawakutanisha viongozi wa Serikali, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchi zinazozunguka Ziwa Tanganyika zikiwemo Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Tanzania ambayo ni mwenyeji.
Waziri Mkuu amesema makongamano ya aina hiyo yana mchango mkubwa katika kuimarisha ushirikiano miongoni mwa mataifa yanayoshiriki.
“Tuna imani kuwa kongamano hili litaibua matumaini mapya ya ushirikiano wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika,” amesema Waziri Mkuu.
“Ukanda huu ndiyo unaongoza kwa madini adimu duniani, na dunia ipo kwenye mwelekeo wa matumizi ya madini haya, hivyo sisi ni matajiri wa madini hayo na hatuna budi kuimarisha ushirikiano ili madini hayo yawanufaishe wananchi. Hivyo ni muhimu kushirikiana kuimarisha na usalama wa ukanda huu; na makongamano kama haya yanachangia pakubwa kuboresha ushirikiano huo kwenye nyanja zote,” amesema.
Waziri Mkuu amesisitiza kuwa mkoa wa Kigoma una fursa na rasilimali nyingi ambazo bado hazijatumika ikiwemo ardhi kubwa yenye rutuba, vivutio vya utalii, madini na viwanda vinavyotoa nafasi ya kuchochea uwekezaji mkoani humo.
Kwa upande wake, Gavana wa Jimbo la Tanganyika la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Christian Kifungwa Muteba ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na nchi hiyo katika nyanja mbalimbali ikiwemo ulinzi na usalama.
Amesema kuwa uwekezaji wa bandari kubwa katika Ziwa Tanganyika utarahisisha usafirishaji wa madini adimu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwenda nchi nyingine bila kulazimika kupitia katika mataifa yaliyo mbali na nchi hiyo.














