Waziri Mkuu wa Tanzania Mwigulu Nchemba amesema nchi hiyo imeweka kipaumbele katika uwekezaji wa viwanda vya dawa nchini ili kupunguza utegemezi wa kuagiza dawa kutoka nje ya nchi.
Akizungumza jijini Nairobi alipokutana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Christophe Lecourtier, kando ya Mkutano wa Ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa (Africa Forward Summit), Nchemba alisema kuwa Tanzania inaagiza kiasi kikubwa cha dawa kutoka nje ya nchi, licha ya kuwepo kwa mpango wa kuwekeza kwenye viwanda vya dawa vya ndani.
“Kupitia ofisi yako pamoja na wadau wengine, wanaweza kutumia fursa hii kubwa iliyopo kuja kuwekeza kwenye eneo hilo. Na kama unavyofahamu, kuwekeza Tanzania ni kuingia katika lango la ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) pamoja na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC),” alisema.
Katika hatua nyingine, Nchemba amepongeza dhamira ya AFD ya kuusaidia Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria Awamu ya Pili, akieleza kuwa mradi huo ni wa kimkakati katika kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
Kulingana na Waziri Mkuu huyo wa Tanzania, serikali yake inaendelea kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo reli ya kisasa ya SGR, nishati, kilimo hususan umwagiliaji pamoja na sekta ya afya kupitia uwekezaji katika uzalishaji wa dawa nchini humo.

















