Nchi za Afrika zaanza kuwarudisha raia wake kutoka Mashariki ya Kati
ULIMWENGU
4 dk kusoma
Nchi za Afrika zaanza kuwarudisha raia wake kutoka Mashariki ya KatiUsafiri wa kwenda na kutoka Mashariki ya Kati unasalia kutatizwa kwani safari za ndege za kibiashara bado hazijaanza, na maelfu wamesalia kukwama wakisubiri msaada kutoka kwa nchi zao.
Kampuni ya Taifa ya Kenya Airways imefanya safari yake ya kwanza kuwarejesha raia wake kutoka Dubai / Reuters
tokea masaa 16

Nchi za Afrika zimeanza kuwarudisha raia wake nyumbani kutoka Mashariki ya Kati.

Mzozo kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran umeongezeka tangu Februari 28, 2026 huku Iran ikiendelea kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Wanafunzi na wafanyakazi wamesafirishwa kutoka Iran na kuwasili katika uwanja wa ndege wa Entebbe siku ya Alhamisi Machi 5, baada ya serikali kuandaa operesheni ya dharura ya kuwarudisha nyumbani.

Serikali ya Uganda nayo imesema raia 43 walikubali usaidizi wa serikali wa kurudi nyumbani, huku kundi dogo likiamua kubaki Mashariki ya Kati.

“Balozi wetu Twaha Matata aliwasiliana na Rais na kupitia, Waziri wa Mambo ya Nje, alitoa kibali cha kuwarudisha wale 43 waliokuwa tayari. Kulikuwa na watu 51 hivi katika chuo kikuu kimoja, lakini wale nane waliamua kubaki kwa ridhaa yao. Serikali ilikuwa tayari kuwarudisha, lakini walibaki," ameelezea Balaam Byaruhanga, Waziri wa Nchi, Jinsia, Kazi na Maendeleo ya Jamii.

Uturuki yawaruhusu kupita

Safari yao haikuwa nyepesi.

Ilianzia katika mji mkuu wa Iran, Tehran, kwa njia ya barabara kwa kutumia basi hadi jijini Istanbul nchini Uturuki na hatimae kupanda ndege kuelekea Uganda.

Serikali ya Uganda imeishukuru Uturuki kwa kuwapa wanafunzi hao viza iliyowaruhusu kuingia na kuendelea na safari ya nyumbani.

Mwanafunzi mmoja anasimulia jinsi mashambulizi yalivyoanza wakati wakijiandaa kuanza kwa muhula mpya wa chuo kikuu.

“Tulikuwa tunaanza muhula mpya Jumamosi. Asubuhi hiyo hiyo, hata hivyo, tulishikwa na mshangao. Kulikuwa na milipuko tena. Na kwa mshangao wetu hatukutarajia yaliyojiri,” Sarah Mayanja mmoja wa wanafunzi hao alielezea.

Hivyo masomo yalikatizwa na wakaanza kutafuta msaada. Hatimae Ubalozi wa Uganda ukapanga taratibu za kidiplomasia za kuwarudisha nyumbani.

Mwanafunzi mwingine ambaye alikuwa amebaki na siku kadhaa kumaliza shahada yake, alisema aliondoka akiwa na hisia tofauti.

"Katika wiki moja tu ya kumaliza masomo yangu, narudi nikiwa na hisia tofauti kwa sababu nilikuwa na siku chache tu kumaliza masomo yangu. Lakini ni bahati mbaya kwamba mambo yalifanyika kwa njia mbaya na ikabidi niondoke kabla ya kumaliza," Jonan Gumushabe alisema.

Kenya yafanya safari yake ya kwanza ya kurejesha raia

Nchini Kenya nako, Shirika la Ndege la Taifa la Kenya Airways limefanya safari yake ya kwanza ya kuwarudisha nyumbani wale waliokuwa wamekwama Mashariki ya Kati tangu kuanza kwa mgogoro huo.

Ndege ya kwanza kutoka Dubai hadi Nairobi, ilitua Machi 5 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi ikiwa na raia wa Kenya.

Awali KQ ilipewa kibali cha kufanya safari moja tu ya kuwachukua abiria waliokwama na kuwarudisha nyumbani.

Miongoni mwa abiria waliorudishwa, kulikuwa na kundi la wanafunzi kutoka shule ya msingi ya Kenya, ambao walikuwa wamekwama Dubai kwa siku tano wakiwa katika ziara ya masomo.

“Tulikuwa karibu na uwanja wa ndege kwa hivyo ilikuwa mbaya,” alilezea Olive Tindika, Mkurugenzi wa Shue ya msingi ya Olivine.

“Mashambulizi hayakutufikia raia lakini tulikuwa tunaona milipuko, tunasikia kelele, munapokea taarifa ya kujificha au watu wanaambiwa wajifiche kwa makazi yao. Ukiwa katika hoteli kama sisi hata hujui mahali pa kukimbilia, hatujawahi kuwa katika hali hiyo,” Tindika alisema.

Nchi nyengine zinafanya mipango

Nchi nyengine za Kiafrika zinaendelea kutoa ushauri wa mara kwa mara kwa raia wake, na kuwataka kukaa katika maeneo yaliyo salama na kujisajili kupitia balozi zao.

Afrika Kusini inasema kuwa inashirikiana na serikali ya Iran kuona ni jinsi gani itawahamisha raia wake waliokwama.

Tayari Waafrika Kusini 6,400 wamejiandikisha katika mfumo maalumu ulioundwa na serikali.

Serikali ya Ghana inasema inajitahidi kuwahamisha raia wake kupitia njia za ardhini.

Nchini Israel, Ghana pia imepunguza uwepo wake wa kidiplomasia na inashughulikia kibali maalum ili kuwahamisha zaidi ya raia wake 900, wakiwemo wanafunzi 65.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria inasema inakamilisha mipango ya kuwahamisha raia wake kutoka maeneo yaliyoathirika.

Usafiri wa kwenda na kutoka Mashariki ya Kati unasalia kutatizwa kwani safari za ndege za kibiashara bado hazijaanza, na maelfu wamesalia kukwama wakisubiri msaada kutoka kwa nchi zao.

CHANZO:reuters