Umoja wa Afrika wataka kukomeshwa kwa mauaji ya Wapalestina

Mwenyekiti huyo wa Tume ya Umoja wa Afrika, pia alitumia fursa hiyo kuangazia migogoro mbalimbali barani Afrika

By
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf./Picha:@EthiopianNewsA

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf ametoa wito wa kukomeshwa kwa mauaji ya Wapalestina yanayoendelea huko Gaza kwa sasa.

"Ni lazima dhamira zetu zitusute kwa yale yanayoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati na Palestina. Mauaji haya ni lazima yakomeshwe," alisema Youssouf, siku ya Jumamosi wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 39 wa umoja huo, unofanyika jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Mwenyekiti huyo wa Tume ya Umoja wa Afrika, pia alitumia fursa hiyo kuangazia migogoro mbalimbali barani Afrika, wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.

"Kuanzia Sudan, kuelekea Sahel, DRC hata Somalia, Waafrika wenzetu wanaendelea kuteseka kutokana na vita,"alieleza.

Mkutano huo unaoanza Februari 14 hadi 15 mwaka huu, unawaleta pamoja wakuu wa nchi 55 kutoka Umoja wa Afrika, chini ya kauli mbiu ya maji safi na mazingira.