Wagombea wote saba wanaowania uongozi wa Umoja wa Mataifa walipokea kura ya "kutopendekezwa" — ambayo kimsingi ni kura ya turufu — kutoka kwa mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kura ya maoni isiyo rasmi ya hivi karibuni, mwanadiplomasia mmoja alisema Ijumaa.
Upigaji kura wa Ijumaa ulikuwa wa kwanza katika mchakato huo wa kura za maoni zisizo rasmi na za siri ambapo Uingereza, China, Ufaransa, Urusi na Marekani zilitumia vijiti vya rangi kuashiria kura zao za turufu, huku wanachama 10 waliochaguliwa katika Baraza la Usalama wakiendelea kutumia alama za kawaida.
Rebeca Grynspan kutoka Costa Rica, ambaye amekuwa mmoja wa wagombea wanaoongoza katika kura tano zilizopita, alipata kura nyingi zaidi za "kuungwa mkono" wakati huu, lakini pia alipata kura tano za "kutopendekezwa," zikiwemo mbili kutoka kwa wanachama wa kudumu.
Ripoti za vyombo vya habari vya Marekani zinaashiria kuwa Washington inapinga wagombea wote saba walio katika kinyang'anyiro hicho.
Wengine wanaweza kujiunga na kinyang'anyiro
Mwakilishi wa Washington katika Umoja wa Mataifa, Mike Waltz, alikataa kutoa maoni kuhusu ripoti hiyo, lakini alisema Ijumaa: "Siku zote tumesema kwamba tunahitaji tu mtu bora zaidi."
Kuhusu uwezekano wa wagombea wapya kujiunga na kinyang'anyiro hicho, Waltz alisema "kama nchi zinataka kuongeza wagombea wengine, hilo bila shaka ni haki yao ya kimsingi ya kitaifa."
Miongoni mwa watu wanaotajwa na wanadiplomasia kama wagombea wanaoweza kujitokeza ni Nickolay Mladenov, mwakilishi mkuu kwa ajili ya Gaza chini ya "Baraza la Amani" linaloungwa mkono na Marekani, pamoja na Lana Nusseibeh, Waziri wa Nchi wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Jina la Feridun Hadi Sinirlioglu kutoka Uturuki, ambaye ni Katibu Mkuu wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya (OSCE), pia limetajwa.
Afrika ina wagombea wawili
Grynspan alifanya vizuri zaidi kwa wastani katika raundi tano za kwanza za upigaji kura usio rasmi, na akaibuka kidedea tena siku ya Ijumaa – licha ya kukabiliwa na kura mbili za turufu (veto).
Wagombea wengine ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Guyana, Carolyn Rodrigues-Birkett; Rafael Grossi wa Argentina, ambaye kwa sasa anaongoza shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia nishati ya nyuklia; Rais wa zamani wa Senegal, Macky Sall; Ivonne A-Baki na Maria Fernanda Espinosa kutoka Ecuador; pamoja na Olara Otunnu wa Uganda.
Katibu Mkuu anayemaliza muda wake, Antonio Guterres kutoka Ureno, atahitimisha muhula wake wa pili wa miaka mitano mnamo tarehe 31 Desemba, 2026.
Hata kama mgombea atapata kura tisa zinazohitajika kati ya kura 15 zilizopo katika Baraza la Usalama, lazima pia aepuke kupigiwa kura ya turufu na mojawapo ya mataifa makuu matano, ambayo kwa sasa yamegawanyika pakubwa.
Uthibitisho wa Baraza Kuu
Mara tu mgombea anapokidhi vigezo hivyo, jina lake litawasilishwa kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa—lenye wajumbe kutoka nchi zote wanachama—ili kuthibitishwa.
Utaratibu wa upigaji kura usio rasmi katika Baraza la Usalama ulianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1980, kwa lengo la kutatua mkwamo uliotokea kati ya wagombea wawili ambao walizuiwa na kura za turufu.
Utaratibu huo usio rasmi umeendelea kuwepo, katika namna mbalimbali, licha ya kukosolewa na nchi zinazopinga mchakato huo ambao hauko wazi.
Kila moja ya nchi 15 wanachama wa Baraza la Usalama inapaswa kumpa kila mgombea—kwa siri—moja ya maoni matatu: "kuhimiza," "kutohimiza," au "kutokuwa na maoni."
Ni desturi kwamba nafasi ya juu zaidi katika Umoja wa Mataifa inapaswa kuzungushwa miongoni mwa kanda mbalimbali duniani.
Kwa msingi huo, nafasi hii inapaswa kwenda kwa mgombea kutoka Amerika ya Kusini wakati huu. Kuna wagombea wengi kutoka kanda hiyo, ingawa Sall na Otunnu wanatoka Afrika.























