Maporomoko ya ardhi yaua watu 102 kusini mwa Ethiopia huku juhudi za uokoaji zikiendelea

Maafisa wa uokoaji kufikia sasa wamefanikiwa kupata miili 52 kutoka kwenye vifusi huku mamlaka zikipeleka vikosi vya dharura na mashine ili kuweza kuwafikia wale walio maeneo ya mbali

By
Kusini mwa Ethiopia. / AA

Idadi ya waliofariki kutokana na maporomoko hayo ya ardhi kusini mwa Ethiopia imefika watu 102, maafisa wa jimbo walisema siku ya Alhamisi, baada ya kutokea tena maafa usiku wa Machi 11 katika eneo la Gamo.

Maporomoko hayo yalikumba wilaya ya Gacho Baba eneo la Gamo baada ya siku kadhaa za mvua kubwa kunyesha na kusababisha maporomoko ya ardhi maeneo ya nyanda za juu.

Ofisi ya mawasiliano ya Gamo inasema pamoja na kuwa idadi ya watu 102 wanaaminika kufariki, juhudi za uokoaji zimefanikiwa kupata miili 52 kufikia sasa kutoka kwenye vifusi.

Tilahun Kebede, msimamizi wa kanda ya Ethiopia Kusini, anasema mamlaka zinaendelea na shughuli za uokoaji pamja na kutoa misaada, akitoa salamu zake za rambirambi wakazi huku akiahidi kuwa usaidizi wa serikali utaendelea.

Maporomoko hayo yamesababisha changamoto kwa waokoaji, ambao kwa sasa wanasema mashine kubwa zinapelekwa huko kwa lengo la kukwangua barabara, na kuruhusu maafisa wa uokoaji kuwafikia wakazi walio katika maeneo ya mbali na msaada wa chakula, dawa na mahema.

Maeneo ya nyanda za juu kusini mwa Ethiopia huwa kwenye hatari ya maporomoko ya ardhi wakati wa msimu wa mvua kubwa nchini humo, ambapo mvua zinazonyesha kwa muda mrefu zinafanya ardhi kuwa nyevunyevu na kutitia.