Buriani Raila Amolo Odinga
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga./Picha:Wengine
Buriani Raila Amolo Odinga
Mwanasiasa huyo mkongwe nchini Kenya amefariki dunia Oktoba 15, 2025 nchini India, alipokuwa akipokea matibabu.
15 Oktoba 2025

Simanzi imetawala nchini Kenya na Afrika Mashariki kwa ujumla, kufuatoa kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Raila Amolo Odinga.

Odinga, mwenye umri wa miaka 80, amefariki dunia nchini India, alipokuwa akipatiwa matibabu.

Raila, maarufu kama ‘RAO’, atakumbukwa kwa ushawishi wake aliokuwa nao kwenye ulingo wa siasa ndani na nje ya Kenya.

Mwanasiasa huyo, aliyezaliwa Januari 7, 1945, amekuwa nguzo muhimu katika historia ya siasa ya nchi hiyo.

Raila, ambaye pia alifahamika kwa jina la ‘Tinga’, amekuwa nguzo muhimu katika siasa za nchini Kenya kutokana na harakati zake za siasa ambazo zimedumu kwa zaidi ya miaka 40.

Kwa kiasi fulani, unaweza kusema kuwa amerithi harakati hizo kutoka kwa baba yake mzazi, Hayati Jaramogi Oginga Odinga, ambaye alikuwa mmoja wa wapigania uhuru wa Kenya na baadaye kuja kuwa Makamu wa Kwanza wa taifa hilo.

Ni harakati hizo hizo, ambazo zilimfanya afungwe jela kwa nyakati tofauti.

Raila, ambaye alipenda kujifananisha na Cesc Fabreags, kiungo mchezeshaji wa zamani wa klabu ya Arsenal, akisisitiza kuwa yeye ni kiungo muhimu katika kutengeneza safu ya uongozi mahiri nchini Kenya.

Mwanasiasa huyo aliwahi kugombea nafasi ya Urais vipindi vitano tofauti, bila mafanikio yoyote.

Licha ya hali hiyo, RAO amekuwa na nafasi na mchango wa pekee kwenye siasa za Kenya.

Kabla ya uchaguzi wa mwaka 2002, chama cha Raila kilijiunga na serikali ya rais wa awamu ya pili Daniel Arap Moi, huku yeye akipewa nafasi ya Uwaziri wa Nishati.

Mwaka 2002 akasaidia upinzani ulioongozwa na rais wa awamu ya tatu Mwai Kibaki kupata ushindi mkubwa dhidi ya Uhuru Kenyatta na chama cha KANU.

 Kugombea Urais

Mwaka 2007 aligombea nafasi ya Urais dhidi ya Mwai Kibaki, ambapo alishindwa na Kibaki, katika matokeo yaliyozua vurugu kubwa baada ya uchaguzi.

Ili kuleta mapatano ndani ya nchi hiyo, Raila ‘akatengenezewa’ nafasi ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Raila aligombea nafasi ya Urais mara mbili; mwaka 2013 na 2017, dhidi ya Uhuru Kenyatta, bila mafanikio yoyote.

Mwaka mmoja baadaye, RAO na Uhuru Kenyatta wakaingia kwenye makubaliano maarufu kama “handshake”, kwa ahadi ya kufanya kazi pamoja na baada ya hapo, Uhuru kumuunga mkono ‘Baba’ katika harakati zake wa kuwania Urais.

Hata hivyo, Raila alipoteza nafasi ya Urais kwenye uchaguzi wa mwaka 2022, aliposimama dhidi ya aliyekuwa Makamu wa Uhuru Kenyatta, William Ruto.

Licha ya kuwa nje ya serikali, mchango wake bado ulionekana baada ya maandamano ya vijana maarufu Gen Z, mwaka 2024, ambapo alionekana kufanya tena “handshake” na serikali ya Ruto, hatua iliyofanya baadhi ya viongozi wa upinzani kujumuishwa kwenye Baraza la Mawaziri.

 Nje ya Siasa

Mbali na siasa, Raila alipenda kusikiliza muziki aina ya Reggae na alikuwa shabiki wa timu ya Arsenal ya nchini Uingereza.

Ameacha mjane, Ida Odinga na watoto watatu Rosemary Odinga, Winnie Odinga na Raila Odinga Jr.

 

CHANZO:TRT Afrika Swahili
Soma zaidi
UN yaagiza uchunguzi wa dharura ufanyike kuhusu ukiukaji wa sheria katika Al Fasher ya Sudan
Rais wa Tanzania atangaza uchunguzi kuhusu mauaji ya waandamanaji katika uchaguzi
Wakimbizi 57,000 wamewasili kaskazini mwa Sudan baada ya mashambulizi ya RSF huko Darfur, Kordofan
Afrika Kusini yaruhusu kuingia kwa wakimbizi zaidi ya 150 kutoka Gaza, Palestina
Afrika yakumbwa na mlipuko wa kipindupindu mbaya zaidi katika miaka 25
Mataifa ya G7 walaani mashambulizi ya RSF dhidi ya raia Sudan, watoa wito wa kusitishwa mapigano
Wakenya zaidi ya 200 wajiunga na jeshi la Urusi
AU yakanusha tuhuma za Trump kuhusu mauaji ya halaiki Nigeria
Mwigulu Nchemba ateuliwa Waziri Mkuu Tanzania
Jaji Mkenya achaguliwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amfuta kazi makamu wake
Duma wa Botswana aipa India zawadi ya duma 8
Kesi ya Roger Lumbala wa DRC yaanza kusikilizwa
Kesi za ubakaji, watoto kupotea zaripotiwa Darfur, Sudan – Umoja wa Mataifa
Ugonjwa wa Kichaa cha mbwa barani Afrika: Janga linaloendelea kuathiri maisha japo linaepukika
Libya yatakiwa kufunga vituo vya kuwazuilia wahamiaji katika mkutano wa Umoja wa Mataifa
Rais Museveni aonya kuzuka kwa vita endapo nchi za Afrika zitashindwa kufikia Bahari ya Hindi
UN: Milioni 11 wanawake na wasichana wanabeba uzito mkubwa wakati njaa ya Sudan inaendelea kupamba moto
Ethiopia yachagguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa, COP32
Ghana yafichua sababu ya ajali ya helikopta iliyoua watu wanane, wakiwemo mawaziri, mwezi Agosti