| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Guterres ashtumu mashambulizi ya kigaidi nchini Mali, atoa wito wa dunia kusaidia
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameshtumu mashambulizi ya kigaidi nchini Mali, akitoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua huku wanaotaka kujitenga wakidhibiti eneo la Kidal.
Guterres ashtumu mashambulizi ya kigaidi nchini Mali, atoa wito wa dunia kusaidia
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameshtumu mashambulizi ya nchini Mali: msemaji / AA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameshtumu mashambulizi ya kigaidi nchini Mali, akitoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia huku vurugu zikiendelea katika eneo la Sahel.

“Katibu Mkuu anaeleza wasiwasi wake kuhusu taarifa za mashambulizi maeneo kadhaa nchini Mali,” msemaji wake ameeleza katika taarifa siku ya Jumamosi.

Guterres ametoa wito “wa msaada kutoka jamii ya kimataifa” kukabiliana na tishio la ugaidi na vurugu katika kanda hiyo, huku akiangazia suala la msaada unaohitajika wa haraka kwa watu.

Kundi lenye uhusiano na Al Qaeda limesema kuwa limeungana na vikosi vya waasi kufanya mashambulizi hayo, ambayo yalianza mapema asubuhi na kuendelea katika maeneo kadhaa.

Waasi wadai kudhibiti Kidal

Waasi wa Azawad Liberation Front (FLA) wanadai kuwa wanadhibiti mji wote wa kaskazini wa Kidal kufuatia operesheni yao.

Kundi hilo linasema kuna sehemu ndogo ambapo wanakabiliana na vikosi vya Mali na mamluki wa Urusi.

Serikali ya Mali ilithibitisha kuhusu mashambulizi katika miji kadhaa, yaliyosababisha watu wasiopungua 16 kujeruhiwa, lakini ikasisitiza kuwa vikosi vya usalama vimechukua tena udhibiti wa maeneo muhimu.

Mamlaka zinaeleza matukio hayo kuwa mashambulizi ya kigaidi, huku vurugu zikiendelea kutikisa uthabiti wa nchi.

FLA inasema operesheni hiyo ilifanywa kwa ushirikiano wa JNIM, kundi lenye uhusiano na Al Qaeda, kama sehemu ya kupanua udhibiti wao kaskazini mwa Mali.

Haikuwezekana kuthibitisha kwa njia huru madai hayo ya FLA.

Mali imekuwa ikikabiliwa na tatizo la usalama tangu 2012, huku vurugu kutoka kwa makundi ya kigaidi, makundi yenye silaha na wale wanaotaka kujitenga zikiwaua maelfu ya watu na raia wengine wengi kuondoka katika makazi yao.

CHANZO:TRT Afrika Swahili