Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni alisema Jumapili kuwa Italia inaandaa hatua mpya zitakazopiga marufuku vifuniko vya uso shuleni na kuweka kikomo cha idadi ya wanafunzi wa kigeni wanaoruhusiwa katika kila darasa.
Meloni alisema hatua hizo zitawasilishwa kwa Baraza la Mawaziri hivi karibuni, huku serikali yake ya mrengo wa kulia ikiongeza mkazo katika masuala ya kutangamana katika jamii na uhamiaji.
Chini ya kanuni hizo zilizopendekezwa, shule zitapiga marufuku mavazi kama vile burqa na niqab, ambayo hufunika uso mzima au sehemu ya uso wa mwanamke. Meloni alisema wanafunzi wanapaswa kuhudhuria shule wakiwa hawajafunika nyuso zao.
Serikali pia inapanga kuweka idadi ya juu ya wanafunzi wa kigeni katika kila darasa, ingawa Meloni hakutaja idadi mahususi.
Alisema sera hiyo ililenga kuwasaidia watoto ambao hawazungumzi Kitaliano kutangamana vyema na mfumo wa elimu; alibainisha kuwa idadi ndogo ya wanafunzi wanaohitaji msaada wa lugha inaweza kujifunza Kitaliano kwa msaada wa walimu na wanafunzi wenzao, huku idadi kubwa ikifanya mchakato huo wa ujumuishaji kuwa mgumu zaidi.
Chini ya hatua hizo zilizopangwa, wazazi wa wanafunzi wa kigeni wanaokabiliwa na changamoto kubwa za kuingiliana na mfumo wa elimu wa Italia watalazimika pia kujifunza lugha ya Kiitaliano.
Raia wa kigeni kwa sasa wanachukua asilimia 11.6 ya wanafunzi waliojiandikisha katika shule za Italia, karibu wanafunzi 12 kati ya kila 100 , kulingana na taasisi ya utafiti ya Fondazione ISMU.
Hapo awali, Italia iliweka vikwazo dhidi ya hijabu zinazofunika uso mzima katika baadhi ya maeneo.
Mwaka 2025, chama cha Meloni cha Brothers of Italy kilianzisha pia mchakato wa kutunga sheria ili kupanua marufuku ya burqa na niqab hadi maeneo ya umma, ikiwemo shule na vyuo vikuu.
Mapendekezo hayo ya hivi karibuni yanakuja wakati masuala ya uhamiaji na ujumuishaji wa wahamiaji, hasa wale wanaotoka nchi zenye idadi kubwa ya Waislamu, yakisalia kuwa mada zenye utata katika siasa za Italia.
Hatua hizo zilizopendekezwa kwa ajili ya shule bado zitahitaji kupitia mchakato wa kutunga sheria nchini Italia kabla ya kuwa sheria rasmi.





















