Erdogan ataka mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Kiev na Moscow kufanyika Istanbul

Rais Erdogan amesema kupitia mkutano ulioandaliwa kwa njia ya mtandao ya kwamba Uturuki iko tayari kuandaa mazungumzo ya moja kwa moja mjini Istanbul na inaendelea kuwasiliana na maafisa wa Ukraine na Urusi.

By
Rais wa Uturuki ajiunga na mkutano kuhusu Ukraine kupitia njia ya mtandaoni.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, alijiunga na mkutano wa mtandaoni wa “Coalition of the Willing” kuhusu Ukraine, kwa mujibu wa Mkuu wa Mawasiliano wa Uturuki, Burhanettin Duran.

“Mkutano huo ulishughulikia yanayojiri katika vita vya Urusu na Ukraine, hatua zilizochukuliwa kuelekea kumaliza mzozo huo, na jitihada zinazoendelea za kuleta amani,” Duran alisema kupitia mtandao wa X siku ya Jumanne.

Alisema Erdogan aliwaambia waliohudhuria mkutano huo ya kuwa Uturuki itaendelea na juhudi za kidiplomasia kuwezesha mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Kiev na Moscow ili kufikia “amani ya haki na ya kudumu” haraka iwezekanavyo.

Kwa mujibu wa Duran, Erdogan pia alisema Uturuki iko tayari kuandaa mazungumzo ya moja kwa moja mjini Istanbul na inaendelea kuwasiliana na maafisa wa Ukraine na Urusu ili kuendeleza lengo hilo.

“Katika mkutano huo, ilielezwa kuwa mpango wa usitishaji mapigano unaojumuisha miundombinu ya nishati na bandari unaweza kutoa mazingira bora kwa mazungumzo ya makubaliano ya kina ya amani kati ya pande husika,” aliongeza.

Wawakilishi kutoka nchi 35 walishiriki katika mkutano huo na kubadilishana maoni kuhusu hatua zinazohitajika ili kuleta amani ya kudumu, Duran alisema.

Wiki iliyopita, Erdogan alitoa wito wa kufufua mazungumzo ya Istanbul ili kumaliza vita kati ya Urusi na Ukraine kufuatia kikao chake na mwenzake wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, nchini Uturuki.

Jumatatu, Erdogan alimwambia Rais wa Urusi, Vladimir Putin, katika mazungumzo ya simu kuwa Ankara itaendelea na juhudi za kusaidia kuhakikisha vita vya Urusi na Ukraine vinamalizika kwa amani ya haki na ya kudumu.

Akizungumza na vyombo vya habari pembezoni mwa mkutano wa viongozi wa G20 Jumapili, Erdogan alisema Uturuki itaendelea kuongeza ushiriki wake katika jitihada za kimataifa za kuleta amani katika maeneo yenye migogoro kuanzia Mashariki ya Kati hadi Afrika na Ukraine, akikazia umuhimu wa Ankara kama mshiriki muhimu katika juhudi za kutatua migogoro ya kimataifa.

Dhamana za usalama

Wakati huo huo, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, akizungumza baada ya mkutano huo wa mtandaoni, alisema Ukraine inahitaji amani ambayo ni “ya kweli” na “inayoheshimu sheria za kimataifa.”

Alisema muungano huo utaanzisha kikundi kazi kitakachoongozwa na Ufaransa na Uingereza, kwa ushirikiano wa karibu na Uturuki na, kwa mara ya kwanza, Marekani, ili kuandaa dhamana za usalama kwa Ukraine mara tu makubaliano ya amani yatakapofikiwa.

“Katika siku chache zijazo, tutakamilisha mchango wa kila upande na kukamilisha dhamana hizi za usalama. Hili ni muhimu kwa Waukraine, ni muhimu kwa kujadiliana amani inayoaminika na kwa kuendelea kuiwekea Urusi shinikizo,” alisema.

Ukraine ilionyesha Jumanne kuwa inaunga mkono muundo wa makubaliano ya amani na Urusi, lakini ikasisitiza kuwa masuala nyeti yanapaswa kushughulikiwa katika mkutano kati ya Rais Volodymyr Zelenskyy na Rais wa Marekani Donald Trump.

Kuhusu mali za Urusu zilizoshikiliwa, Macron alisema: “Tutakamilisha hili katika siku zijazo, kwa ushirikiano na nchi zote za Ulaya zinazohusika zaidi na, bila shaka, Umoja wa Ulaya na Tume ya Ulaya, ili kupata suluhisho litakalohakikisha ufadhili, kutoa matumaini ya kifedha kwa Ukraine na kuendelea kuweka shinikizo hili.”