Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali imeridhishwa na hatua iliyofikiwa ya maandalizi ya ujenzi katika mradi wa kimkakati wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Machi 22, 2026, alipokutana na Mwenyekiti wa Kampuni ya China Harbour Engineering Company Limited, Bai Yinzhan, pamoja na ujumbe wake waliofika Ikulu, Zanzibar.
Amesema maendeleo ya mradi huo yana umuhimu mkubwa kwa uchumi wa Zanzibar.
Aidha, Rais Mwinyi ameeleza kuwa hatua iliyofikiwa kwa sasa inatoa matumaini ya kuona sura halisi ya mradi huo ifikapo Septemba 2026, ambapo awamu ya kwanza ya mradi inatarajiwa kukamilika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kampuni ya China Harbour Engineering Company Limited, Bai Yinzhan, amemuhakikishia Rais Mwinyi kuwa kampuni hiyo inaendelea na ujenzi kwa kasi huku ikizingatia viwango vya ubora, ikitambua umuhimu wa mradi huo kwa maendeleo na uchumi wa Zanzibar.
Aidha, amepongeza ushirikiano mzuri wanaoupata kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Rais Mwinyi anatarajiwa kuweka jiwe la msingi la mradi wa kimkakati wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani leo.













