Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imefikia 600, kulingana na takwimu zilizotolewa mwishoni mwa Jumatano na Wizara ya Afya ya nchi hiyo.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa maambukizi yaliyothibitishwa ya Ebola yamefikia 1,759, huku maambukizi ya ugonjwa huo yakiendelea kuenea katika jamii.
Mlipuko huo wa aina ya virusi vya Bundibugyo umejikita katika maeneo 37 ya huduma za afya yaliyopo katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini, na Kivu Kusini.
Hata hivyo, taarifa za hivi karibuni zimeonyesha kuwa watu wawili wengine waliogunduliwa kuambukizwa na ugojnwa huo mjini Kisangani, katika jimbo la Tshopo, yanahusishwa na kituo cha afya cha Nia-Nia kilichopo Ituri.
Jumla ya watu 750 wamepona ugonjwa huo, huku wagonjwa 285 wakiendelea kupatiwa matibabu.
Ofisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya Afrika ilisema Jumanne kuwa mlipuko huo unaendelea kushuhudia ongezeko la vifo vinavyotokea katika jamii pamoja na kusambaa kwa maambukizi katika vituo vya afya ambavyo hapo awali havikuwa vimeathirika, hasa katika majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini.
Jimbo la Ituri linaendelea kuathirika zaidi wa mlipuko huo, likichangia zaidi ya asilimia 90 ya maambukizi yote na zaidi ya asilimia 84 ya vifo tangu mlipuko huo ulipotangazwa rasmi Mei 15.
WHO imeonya kuwa idadi kubwa ya vifo vinavyoripotiwa kabla ya wagonjwa kufikishwa katika vituo vya matibabu inaonyesha kuwa mifumo ya ufuatiliaji wa wagonjwa na rufaa bado haijaendana na kasi ya maambukizi.
Kati ya vifo 430 vilivyothibitishwa na kufanyiwa uchunguzi hadi Julai 5, WHO ilisema takriban vifo 400 vilitokea kabla ya wagonjwa kulazwa katika vituo vya matibabu, hali inayodhihirisha ucheleweshaji unaoendelea katika kubaini maambukizi, kutenga wagonjwa na kuhakikisha wanapata huduma za matibabu kwa wakati.












