Utajiri wa Afrika: Almasi ya Jangwani
Soko la mitindo ya kisasa linaanza kuikumbatia aina nyingine ya almasi, inayoitwa "Almasi ya jangwani," au “Desert diamonds” ambayo inavaliwa kwa asili yake bila kuboreshwa
Kihistoria almasi ina thamani kubwa, mtu anahisi kuthaminiwa zaidi pindi anapopewa zawadi ya almasi.
Tunajua almasi ina rangi ya manjano isiyokolea na kahawia na nyengine kutokuwa na rangi ambazo ni adimu zaidi, na hivyo kuwa na thamani zaidi.
Lakini sasa soko la mitindo linaanza kuikumbatia aina nyingine ya almasi, inayoitwa "Almasi ya jangwani," au “Desert diamonds” kwa Kiingereza.
Almasi ya jangwani hutolewa na kuundwa katika umbo lake la asili, bila kusafishwa au kuboreshwa.
Ni almasi asilia ambayo inatokana na joto miaka mingi iliyopita, na kupata rangi yake ya kipekee kutokana na mazingira asili.
Na almasi za jangwani sasa zinawavutia watu maarufu, walio kwenye tasnia ya urembo na matajiri ambao sasa wanatafuta "vitu tofauti."
Na utajiri wote huu unatoka Afrika, hasa Namibia na Botswana.
Botswana ndio mzalishaji mkubwa zaidi wa almasi duniani kwa thamani na ya pili kwa uzito (karati).
Kufikia 2025, nchi hi ya Kusini mwa Afrika ilikuwa na wastani wa karati milioni 250 katika hifadhi yake ya almasi.
"Almasi za Jangwa" nchini Botswana zinatoka kwenye Jangwa la Kalahari. Almasi hizi hutolewa mahsusi kutoka katika migodi iliyoko katika maeneo kame, yaliyofunikwa na mchanga katikati na kusini mwa Botswana.
Namibia nayo ni kati ya wazalishaji kumi bora kimataifa wa almasi zenye ubora wa juu ambapo mwaka 2025, ilizalisha karati milioni 2.082 ya almasi.
Almasi hapa hupatikana baharini na inachimbwa kwa kutumia vyombo vya juu.
Lakini hii "Almasi ya jangwani" nchini Namibia inapatikana katika pwani ya nchi hiyo.
Kundi la De Beers ambalo ni kampuni kubwa ya uchimbaji wa almasi nchini Namibia na Botswana lilianza kuipa umaarufu "almasi ya jangwani" katika soko la kimataifa tangu mwaka 2025, ikitilia mkazo uzuri wake wa kiasili ambao ni adimu.
Watu mashuhuri ambao wamevaa “almasi za Jangwani” hivi karibuni ni pamoja na Sarah Paulson, mshindi wa Oscar Jessie Buckley, na msanii Taylor Swift ambaye pete yake ya uchumba ilitengezwa na vito adimu vya almasi ya jangwani.
Kulingana na De Beers, utafiti wake uligundua kuwa 90% ya watumiaji walionesha nia ya kununua “Almasi ya Jangwa” kama njia ya kupata muonekano tofauti na kuonyesha uhusiano wa moja kwa moja na mazingira asili.
Wataalamu wanasema ukuaji wa soko la almasi hii ya asili huenda ukasaidia kupunguza matumizi ya almasi iliyotengenezwa katika maabara ambayo inatishia kuchukua soko la mawe haya ya asili.