Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepongeza makubaliano yaliyofikiwa na makundi hasimu ya kisiasa nchini Libya ambayo yanatoa fursa kwa uchaguzi kufanyika katika kipindi cha miaka miwili ijayo.
Makubaliano hayo yanayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, yaliyotiwa saini mjini Tripoli Agosti 30, yametajwa kuwa hatua muhimu katika kuelekea kuwa na uchaguzi wa kitaifa kwenye nchi hiyo iliyogawanyika kiitikadi.
Jerome Bonnafont, balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, ambaye ndiye anayeongoza Baraza la Usalama mwezi huu, siku ya Jumanne aliyataja makubaliano hayo kwamba ni "hatua muhimu kuelekea katika kuwa na uchaguzi wa kitaifa ulio huru, haki, na wazi", pamoja na "kuimarisha umoja wa taasisi za Libya kutimiza azma ya watu wa Libya."
Bonnafont alisisitiza umuhimu wa "makubaliano kuungwa mkono na wadau wote wa Libya, na kuwahimiza kushirikiana katika utekelezaji wake."
Baraza la Usalama lilieleza "kumuunga mkono kikamilifu" Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Libya Hanna Tetteh, Bonnafont aliongeza.
Taifa hilo la Afrika Kaskazini lenye utajiri wa mafuta limekuwa na wakati mgumu kujikwamua kutoka kwenye vurugu zilizompindua kiongozi wake wa muda mrefu Muammar Gaddafi.
Mchakato huo, ulioanzishwa Agosti 2025 na Umoja wa Mataifa, unatoa wito wa kuwepo kwa mifumo ya uchaguzi nchini humo, kuunganisha taasisi za uongozi zilizogawanyika na kuwepo kwa majadiliano ya kisiasa.




















