Wasomali wakamatwa Minneapolis katika msako dhidi ya wahamiaji

Maafisa hawakutoa idadi kamili ya watu waliokamatwa, lakini walitoa wasifu wa watu 12 waliokamatwa, watano wao wakiwa ni Wasomali, na wengine kutoka Mexiko na El Salvador.

By
Hali ya wasiwasi kwa jamii ya Minnesota huku kukiwa na ripoti ya operesheni ya serikali ya Marekani dhidi ya wahamiaji. / / Reuters

Watu wenye asili ya Kisomali ni miongoni mwa waliokamatwa katika operesheni dhidi ya wahamiaji mjini Minneapolis, Marekani, maafisa wa serikali kuu walisema siku ya Alhamisi, siku mbili baada ya Rais Donald Trump kutoa maneno makali dhidi ya wahamiaji kutoka nchi ya Pembe ya Afrika na kudai anataka wafukuzwe kutoka nchini humo.

Msako huo ulianza siku ya Jumatatu, kwa mujibu wa taarifa ya kwanza ya wizara ya mambo ya ndani kuhusu operesheni hiyo.

Maafisa hawakusema kuhusu idadi kamili ya waliokamatwa, lakini walitoa taarifa za watu 12 waliozuiliwa, watano wao wakiwa Wasomali na wengine kutoka Mexico na El Salvador.

Katika taarifa hiyo, Naibu Msemaji Wizara ya Mambo ya Ndani, Tricia McLaughlin, aliwataja wote kama wahalifu hatari wenye makosa mbalimbali, kuanzia udanganyifu na wizi wa magari hadi udhalilishaji wa kijinsia na kuendesha gari wakiwa walevi.

Upendo na heshima

Meya wa Minneapolis, Jacob Frey, kutoka chama cha Democrat, amelaani vikali mashambulizi ya Trump dhidi ya jamii ya Wasomali wa jiji hilo na siku ya Alhamisi alitoa wito kwa Wamarekani “kuwapenda na kuwaheshimu.”

Jamii ya wahamiaji wa Kisomali nchini Minnesota ndiyo kubwa zaidi Marekani Kaskazini.

Kauli za kibaguzi za Trump dhidi ya Wasomali, pamoja na mashambulizi yake dhidi ya wanasiasa wa Minnesota wanaowatetea, zimepongezwa na wafuasi wake.

Siku ya Jumanne, katika mkutano wa televisheni wa baraza la mawaziri, alijibu taarifa za madai ya udanganyifu serikalini miongoni mwa baadhi ya wanajamii wa Kisomali kwa kuwaita wahamiaji hao “takataka” na kusema anataka warudishwe “walikotoka.”

Hotuba za kupinga uhamiaji zilikuwa sehemu kubwa ya kampeni ya Trump. Tangu aingie madarakani Januari, ameongoza oparesheni kali za maafisa wa serikali kii waliojificha uso kote nchini, akilenga kuongeza kuwarudisha wahamiaji makwao. Kadiri muda unavyosonga, lugha anayoyatumia hadharani kuhusu wahamiaji imekuwa kali zaidi.

Msako wa New Orleans

Vile vile siku ya Alhamisi, maafisa wa serikali kuu walisema wamekamata makumi ya watu huko New Orleans, jiji jingine linaloongozwa na Democrats.

Siku ya pili ya oparesheni ya New Orleans, waandamanaji walivuruga kikao cha baraza la jiji wakidai madiwani watangaze maeneo ya jiji kuwa “maeneo yasiyo na ICE,” ambako maafisa wa uhamiaji wa serikali kuu hawataruhusiwa kufanya shughuli za kuwakamata wahamiaji.

Waandamanaji walituhumu maafisa wa serikali kuu kuwajeruhi au kuwalenga watu wa rangi bila kubagua, wakiwemo raia wa Marekani wasiokuwa na rekodi ya makosa ya jinai—mashitaka ambayo DHS imeyakanusha.

Meya mteule wa New Orleans, Helena Moreno, alisema Jumatano kwamba oparesheni hiyo imeleta hali ya hofu miongoni mwa wakazi walio hatarini zaidi.

“Lazima tufanye yote tuwezayo kulilinda jiji la New Orleans na kuhakikisha kuwa mchakato wa haki unafuatwa kwa wakazi wote,” alisema, akitangaza mfumo wa mtandaoni kwa raia kuripoti unyanyasaji wa maafisa wa uhamiaji.

Gavana wa Louisiana, Jeff Landry, kutoka chama cha Republican, ameunga mkono juhudi za utekelezaji wa sheria za uhamiaji za serikali kuu.