Elimisha msichana, elimisha jamii.
Kupitia mradi wa ‘Binti Shupavu’, jumla ya baiskeli 100 zilitolewa kwa wanafunzi waliopo mkoa wa Morogoro./Picha: GLAMI / Others
Elimisha msichana, elimisha jamii.
Shirika la Umoja wa Mataifa, Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) linasema kuwa ni asilimia 39 tu ya wasichana wa Kitanzania ndio wanaokwenda shule za sekondari huku chini ya asilimia 3 wakipata fursa kwenye elimu ya juu.

Elimisha msichana, elimisha jamii. Ni kauli maarufu yenye kuweka msisitizo kwenye umuhimu wa kuwapa watoto wa kike, haki ya kupata elimu kwa manufaa mazima ya jamii husika.

Inasemekana kuwa, iwapo mtoto wa kike akipata fursa ya kupata elimu, basi jamii yake itapata manufaa makubwa.

Hata hivyo, licha ya jitihada mbalimbali za serikali za kuhakikisha kuwa watoto wa kike wanapata elimu, bado idadi kubwa ya wanafunzi hao wanashindwa kuendelea na masomo yao.

Nchini Tanzania, shirika lisilo la kiserikali la Girls Livelihood and Mentorship Initiative (GLAMI), limechukua jukumu la kuwasaidia watoto wa kike kupata elimu.

GLAMI hutekeleza majukumu hayo kupitia Programu yake miwili ya Kisa na Binti Shupavu.

Kukosa masomo ya darasani

Programu ya ‘Binti Shupavu’ huwapatia wanafunzi wa kike elimu ya stadi za maisha ikiwemo kujitambua ili kumsaidia mtoto wa kike kukabiliana na changamoto anazoweza kukumbana nazo kwenye safari yake ya elimu.

Programu hiyo ni hatua mojawapo ya kufanikisha lengo namba 4 la malengo ya maendeleo endelevu duniani.

Hata hivyo, changamoto ya umbali wa shule unasababisha wengi wa mabinti hao kukosa masomo.

“Kila siku naamka saa 10 alfajiri na kuanza safari ya saa tatu hadi kuelekea shule, ambapo mara kwa mara nalazimika kukosa vipindi viwili vya awali darasani kwani huwa nafika shuleni saa tatu asubuhi,” anaeleza Zubeda Shabani (si jina lake halisi).

Ukosefu wa masomo kwa wanafunzi kama Zubeda umekuwa na athari kubwa kitaaluma.

Wapo wanaoshindwa kufanya vizuri darasani, na wapo wanaolazimika kukatisha masomo.

Pia, wapo wanaofika shuleni wakiwa wamechoka kutokana na kutembea umbali mrefu, na kushindwa kufuatilia vipindi vya darasani katika hali ya utimamu.

‘Nyonga’ mpaka darasani

Baada ya kuguswa na changamoto hiyo, shirika la GLAMI, kwa kushirikiana na ABC Impact, hivi karibuni walianzisha mkakati uitwao “Ride To The Future”.

Mpango huo unalenga kuwapatia nyenzo wanafunzi wa kike, ambazo ni baiskeli zitakazo wawezesha kuwahi vipindi shuleni.

Kupitia Programu ya ‘Binti Shupavu’, jumla ya baiskeli 100 zilitolewa kwa wanafunzi waliopo mkoa wa Morogoro.

 “Huu ni mwanzo tu wa safari yetu,” anasema Einoth Justine, Msimamizi wa Programu ya ‘Binti Shupavu’ mkoani Morogoro,

Kulingana na msimamizi huyo, wanafunzi wapatao 332 bado wanakabiliana na changamoto ya kutembea umbali mrefu wa kuelekea shuleni kila siku.

“Mpango bado unaendelea, tukiwa tumejiwekea lengo la kutafuta baiskeli nyingi zaidi huku shule tano zikiwa tayari zimenufaika na Programu hiyo,” anaeleza.

Baadhi ya shule hizo ni pamoja na Gwata, Ngerengere, Bwakila Chini, Kisaki na Majimoto, ambazo ziko halmashauri ya Morogoro vijijini.

Taasisi ya ABC Impact imeendesha mafunzo ya matumizi ya baiskeli hizo pamoja na matengenezo yake.

“Tunafahamu changamoto ambazo watoto wa kike wanakutana nazo,” anaeleza Mohammed Musa, Meneja Mradi wa ABC Impact.

 “Kuna nyakati watoto wa kike hupakiwa kwenye baiskeli na watu wasio wafahamu, hii inaweza kusababisha ndoa za utotoni hata kuacha masomo,” anaongeza Musa.

Tayari kutimiza ndoto

Kwa sasa, Zubeda yupo tayari kufanya vizuri kwenye masomo yake kufuatia msaada wa baiskeli.

 “Ninashukuru sana kwa baiskeli hii, kwa sasa sitokuwa na hofu yoyote ya kukosa masomo darasani, nikiamini kuwa lengo la kutimiza ndoto yangu maishani haiko mbali,” anasema.

Shirika la Umoja wa Mataifa, Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) linasema kuwa ni asilimia 39 tu ya wasichana wa Kitanzania ndio wanaokwenda shule za sekondari na chini ya asilimia 3 wanakwenda elimu ya juu.

Programu ya ‘Binti Shupavu’ ulizinduliwa mwaka 2017 mkoani Kilimanjaro, ukilenga kusaidia wasichana wenye umri wa miaka 12 hadi 18.

CHANZO:TRT Afrika