Kwa nini biashara isiyo halali ya siafu inaongezeka?
Ukusanyaji wa mchwa umeanza kuwa maarufu katika miaka ya hivi karibuni katika nchi za Ulaya, China na Vietnam.
Mahakama nchini Kenya 17 Machi 2026, iliwashtaki wanaume wawili kwa kusafirisha wanyamapori kinyume cha sheria baada ya mmoja wao, raia wa China kukamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi akiwa na siafu zaidi ya 2,000.
Zhang Kequn, 27, alizuiliwa alipokuwa akijaribu kuondoka nchini, nyaraka za mahakama zilionyesha.
Maafisa wa uhamiaji wa Kenya walikuwa wameashiria hati yake ya kusafiria likuwa imewekwa ilani yakusimanmishwa baada ya kukwepa kukamatwa nchini humo 2025.
Kulingana na Mamlaka ya Wanyamapori ya nchi hiyo, ukusanyaji na usafirishaji wa siafu bila idhini ni ukiukaji wa sheria za kitaifa za bayoanuwai na kanuni za kimataifa.
Waendesha mashtaka walimshtaki mtu wa pili, Charles Mwangi, wakimshtumu kwa kusambaza siafu kwa wafanyabiashara wa kigeni.
David Lusweti wakili wa Zhang alielezea mahakama hiyo,
" Zhang amenidokeza kwamba alikuwa tu akisafirisha siafu hao ,Yeye si mmiliki wa wadudu hao, bali amesema kuwa Mkenya huyo ndiye alikuwa akiwatafuta siafu hao na kumuuzia."
Maafisa wa usalama walimhusisha Mwangi na shehena ya siafu walionaswa huko Bangkok mnamo Machi 10, ambayo ilitoka katika mji wa bandari wa Mombasa nchini Kenya.
Kwa nini biashara ya siafu?
Ukiona siafu unawaua au kuwafukuza ili wasikung'ate, lakini unajua kuna watu kazi yao ni kuwakusanya?
Maonesho maalumu ya siafu huandaliwa huko Asia na Ulaya ambapo mashabiki huvutiwa kwenda kuangalia.
Wengine wanaamini kuwa kuwaangalia siafu wakiwa katika makoloni yao ni aina ya matibabu.
Imekuwa ni biashara kubwa kupitia tovuti mbalimbali zinazouza spishi za siafu, ikijumuisha wale wanaotolewa Afrika.
Changamoto inayojitokeza sasa, ni kuibuka kwa wimbi la wasafirishaji kinyume cha sheria.
Ongezeko ya biashara haramu
Kumekuwa na kesi nyingi nchini humo za walanguzi kukamatwa.
Mnamo Mei 2025, watu wanne walipatikana na hatia ya kujaribu kusafirisha siafu 5,440 kutoka Kenya hadi Ulaya na Asia.
Washukiwa hao kutoka Ubelgiji, Vietnam na Kenya walitozwa faini ya Dola za Marekani 7700 kila mmoja au watumikie kifungo cha mwaka mmoja.
Walinaswa wakiwa na mkusanyo wa siafu malkia wenye thamani ya dola za Marekani 9300 wakati huo, huku kila mdudu akiripotiwa kuwa na thamani ya dola za Marekani 233.
Iwapo wangefanikiwa kuwasafirisha, basi uchukuzi huo ungewaletea dola za Marekani 1,267,520.
Mnamo 2023, Wakenya watatu vile vile walishtakiwa kwa kujaribu kupeleka nchini Ufaransa siafu wenye thamani ya Dola za Marekani 2,321 kinyume cha sheria.
Wataalamu wanaonya kwamba, ingawa siafu wanauzwa kama wadudu wanaopendwa duniani kote, lakini wakianzishwa nje ya safu zao asili wanaweza kuwa vamizi na kuleta athari mbaya kwa mazingira.
Pia wanatahadharisha kuwa kuwasafirisha siafu malkia ambao ni muhimu katika maisha ya makoloni kunaweza kuhatarisha makundi ya siafu kuleta madhara kwa viumbe hai.