Raia wa Uturuki na wanaharakati wengine wa mataifa mbalimbali waliokuwa ndani ya meli za msafara wa misaada ya kibinadamu wa Global Sumud uliokamatwa na Israel katika maji ya kimataifa wanatarajiwa kuwasili Uturuki leo kwa ndege maalum, maafisa wa Uturuki walisema Ijumaa.
“Kutokana na hatua zisizo halali zilizochukuliwa na vikosi vya Israel dhidi ya msafara wa Global Sumud katika maji ya kimataifa, raia wetu na washiriki wengine waliokuwa wamekamatwa wameteremshwa katika kisiwa cha Krete,” aliandikka msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki, Oncu Keceli, kwenye mtandao wa X.
“Balozi wetu wa nchini Ugiriki na wafanyakazi wetu wa ubalozi wako Krete. Raia wetu na baadhi ya washiriki wa mataifa mengine wanatarajiwa kusafirishwa Uturuki leo kwa ndege maalum,” aliongeza.
Msafara wa Global Sumud umetoa wito kwa serikali kuishinikiza Israel kuwaachia waliokamatwa kutoka katika misheni yake iliyokuwa ikielekea Gaza, ukisema wanaharakati wawili bado wanashikiliwa.
Katika taarifa, kundi hilo limesema washiriki wengi waliokuwa wamezuiliwa wameachiliwa huko Krete, lakini watu wawili — waliotambuliwa kama Thiago na Saif — bado wanazuiliwa.
“Tunaomba serikali zote zifanye kila liwezekanalo kuishinikiza serikali ya Israel kuwaachilia huru wote waliotekwa kinyume cha sheria,” msafara huo ulisema.
Siku ya Alhamisi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel ilisema wanaharakati 175 walizuiliwa baada ya zaidi ya meli 20 kukamatwa katika maji ya kimataifa wakati zikielekea Gaza.
Msafara huo, uliobeba misaada ya kibinadamu kwa Gaza, unalenga kuvunja mzingiro wa Israel na kufungua njia ya misaada kwa njia ya bahari.
Misheni hii ni jaribio la pili la Global Sumud Flotilla, baada ya juhudi ya awali mnamo Septemba 2025 iliyomalizika kwa kuzuiwa na Israel katika maji ya kimataifa na kukamatwa kwa mamia ya wanaharakati wa nchi mbalimbali.
Mnamo Oktoba 2023, Israel ilianzisha vita vya mauaji ya halaiki huko Gaza, ambavyo vimeua zaidi ya Wapalestina 72,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuharibu takriban asilimia 90 ya miundombinu ya eneo hilo, huku gharama za ujenzi upya zikikadiriwa na Umoja wa Mataifa kuwa takriban Dola bilioni 70.
Israel imekuwa ikiweka mzingiro dhidi ya Gaza tangu mwaka 2007.













