Mkuu wa Majeshi wa Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba amesema kuwa nchi yake ipo tayari kuisaidia Israel katika vita vya Mashariki ya Kati, iwapo taifa hilo litashindwa.
“Tunataka kuona vita vya Mashariki ya Kati vikiisha mara moja kwani dunia imeshachoka sasa. Hata hivyo, hatutosita kuingia vitani na kuisaidia Israel iwapo taifa hilo litaonekana kushindwa mapambano,” aliandika Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni, kupitia mtandao wa X, siku ya Jumatano.
Kauli ya Jenerali Muhoozi inakuja huku vita vya Marekani-Israel dhidi ya Iran vikiendelea kupamba moto katika eneo la Mashariki ya Kati.
Katika hatua nyingine, Kainerugaba ametangaza mpango wake wa kujenga sanamu ya Yonatan “Yoni” Netanyahu, ambaye ni ndugu yake Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambaye aliuawa wakati wa harakati za kuwakomboa mateka katika uwanja wa ndege wa Entebbe, mwaka 1976.








