Maafisa 2 wa Kenya wamefariki baada ya gari lao kukanyaga bomu lililotegwa na kundi la al-Shabab

Maafisa wawili wa Kikosi cha Ulinzi wa Mipakani nchini Kenya wamefariki siku ya Jumatano baada ya gari lao kukanyaga bomu lililotegwa ardhini (IED) na wanamgambo wa al-Shabab wanaotoka Somalia, kwa mujibu wa polisi wa Kenya.

By
Mamlaka za Kenya zinasema al-Shabab bado ni tishio kubwa, hususan kupitia mabomu ya kutegwa ardhini. /

Shambulio hilo lilitokea karibu na mpaka wa Kenya na Somalia katika Kaunti ya Garissa, eneo lililo takriban kilomita 370 kaskazini mashariki mwa mji mkuu, Nairobi.

Maafisa wa polisi waliozungumza na wanahabari walisema wanachama wa al-Shabab walitega na kulipua kifaa hicho wakati maafisa hao wakiwa doria, na kuliharibu kabisa gari lao na kuwaua papo hapo.

Vikosi vya usalama vimetumwa kulidhibiti eneo hilo, ambako kundi hilo la wapiganaji limekuwa likiwalenga mara kwa mara maafisa wa usalama na kuvuruga shughuli za ulinzi mpakani.

Picha kutoka eneo la tukio zinaonyesha gari la doria lililosambaratika na kupinduka upande mmoja, vipande vya chuma vilivyosambaa barabarani, na shimo kubwa linaloaminika kuwa sehemu ya mlipuko; maafisa pia walionekana wakichunguza mabaki hayo.

Kenya imekuwa ikishambuliwa mara kwa mara na al-Shabab tangu ilipotuma wanajeshi Somalia mwaka 2011 chini ya Kikosi cha Umoja wa Afrika (sasa ATMIS).

Kundi hilo la kigaidi mara nyingi hufanya mashambulizi ya kuvizia mpakani, kulipua mabomu barabarani hasa yakilenga doria za polisi, na kushambulia vituo vya polisi vilivyo maeneo ya ndani, kwa lengo la kuishinikiza Kenya iondoe wanajeshi wake Somalia.

Kaunti za Garissa, Mandera na Wajir, zinazopakana na Somalia ndizo zimeathiriwa zaidi, huku al-Shabab wakitumia mianya katika mipaka, miundombinu duni ya barabara na mazingira ya mbali ili kufanya mashambulizi.

Licha ya doria kuongezwa na uangalizi kuimarishwa, mamlaka za Kenya zinasema al-Shabab bado ni tishio kubwa, hususan kupitia mabomu ya kutegwa ardhini (IED), ambayo yameua makumi ya maafisa wa usalama katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.