Baada ya ziara iliyokuwa na mabishano ya wazi kati ya Papa Leo na Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu vita, Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duaiani alizihimiza Marekani na Iran kurejea kwenye mazungumzo.
Alitoa wito wa kuanzishwa kwa “utamaduni mpya wa amani” kuchukua nafasi ya vurugu kila mara migogoro inapozuka.
Kulingana na Kiongozi huyo, suala muhimu si kama utawala wa Iran unapaswa kubadilika au la. “Swali linapaswa kuwa jinsi ya kukuza maadili tunayoyaamini bila kusababisha vifo vya watu wengi wasio na hatia.”
Alifichua kwamba hubeba picha ya mvulana Muislamu kutoka Lebanon aliyeuawa katika vita vya hivi karibuni vya Israel na Hezbollah. Mvulana huyo alikuwa amepigwa picha akiwa ameshika bango la kumkaribisha Papa alipokuwa ameitembelea Lebanon mwaka uliopita.
“Kama mchungaji siwezi kuunga mkono vita,” aliwaambia waandishi wa habari akiwa ndani ya ndege yake. “Ningependa kuhimiza kila mtu kutafuta majibu yanayotokana na utamaduni wa amani badala ya chuki na mgawanyiko.”
Alipoulizwa kama analaani mauaji ya hivi karibuni ya Iran, Papa Leo alisema analaani “vitendo vyote visivyo vya haki” na akaijumuisha adhabu ya kifo katika orodha hiyo.
“Ninalaani kuuliwa kwa watu. Ninalaani adhabu ya kifo. Ninaamini maisha ya binadamu yanapaswa kuheshimiwa, na kwamba watu wote tangu kuzaliwa hadi kufa (kifo cha kawaida), maisha yao yanapaswa kuheshimiwa na kulindwa.
“Hivyo basi, pale ambapo utawala au nchi inachukua maamuzi yanayoondoa maisha ya watu wengine bila haki, basi wazi hilo ni jambo linalopaswa kulaaniwa,” alisema.

















