Nchi ya Kuwait imesema mifumo yake ya ulinzi inakabiliana na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani , huku washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba wakiendelea kuwa katika hali ya tahadhari. Hali hiyo imejitokeza saa chache baada ya Marekani kufanya shambulizi katika Kisiwa cha Qeshm, nchini Iran, kilichopo kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz.
Nayo nchi ya Bahrain imesema mifumo yake ya ulinzi wa anga ilifanikiwa kuzuia mashambulizi yaliyotoka Iran mapema Jumatano. Tukio hilo limetokea siku moja baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran kutangaza kuwa lilishambulia kambi ya kijeshi iliyopo Bahrain, ambayo hutumiwa na Marekani.
Jeshi la Kuwait limetoa taarifa Jumatano likisema mifumo yake ya ulinzi wa anga inaendelea kukabiliana na vitisho vya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kutoka kwa kwa wale aliyowaita maadui. Jeshi hilo pia limewataka wananchi kufuata maelekezo ya kiusalama na tahadhari yanayotolewa na mamlaka husika.
Awali, Shirika rasmi la Habari la Iran (IRNA), likimnukuu afisa mmoja wa kikanda, liliripoti kuwa Marekani ilishambulia Kisiwa cha Qeshm, lakini shambulizi hilo halikusababisha uharibifu mkubwa.
Afisa mmoja wa Marekani aliyezungumza na Shirika la Habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina alisema ndege za kivita za Marekani zilitumia silaha zinazoongozwa kwa usahihi kulenga eneo la kurushia makombora la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) katika Kisiwa cha Qeshm.
Afisa huyo aliongeza kuwa shambulizi hilo lilikuwa sehemu ya hatua ya kujibu mashambulizi ya Iran.



















