| Swahili
AFRIKA
3 dk kusoma
Nigeria yaitaka Afrika Kusini kuchukua hatua zaidi dhidi ya vurugu zinazowalenga wahamiaji
Mamlaka za Nigeria zinasema kuwa polisi wa Afrika Kusini walionekana kutokuwa tayari kuwalinda raia wa kigeni, ingawa serikali ya Afrika Kusina inasema inapinga chuki dhidi ya wageni.
Nigeria yaitaka Afrika Kusini kuchukua hatua zaidi dhidi ya vurugu zinazowalenga wahamiaji
Wafuasi wa kundi la Afrika Kusini linalopinga wahamiaji, 'March and March', wakiandamana katika eneo la Umzimkhulu, Afrika Kusini. / / Reuters

Nigeria imeitaka Afrika Kusini kuchukua hatua zaidi kuzuia mashambulizi dhidi ya raia wa Nigeria na wahamiaji wengine wa nchi za Afrika, ikisema kuwa vurugu zinazojirudia zimekuwa zikiharibu uhusiano kati ya nchi hizo na kuzua maswali kuhusu iwapo serikali ya Afrika Kusini inahusika kwa namna fulani au inazifumbia macho.

Kauli hizo zilitolewa wakati wa mazungumzo yaliyofanyika mjini Abuja kati ya maafisa wa Nigeria na wajumbe wa Afrika Kusini walioongozwa na Mjumbe Maalum na Waziri wa Mahusiano ya Kimataifa, Ronald Lamola.

Vyombo vya habari vya Nigeria viliripoti kuwa Rais Bola Tinubu alikataa kuupokea ujumbe huo uliotumwa na mwenzake wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, na badala yake akauelekeza kukutana na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Sola Enikanolaiye.

Msemaji wa Rais Tinubu amenukuliwa akithibitisha hatua hiyo ya kidiplomasia, jambo linaloashiria kuzorota kwa uhusiano kati ya nchi hizo kufuatia wimbi la hivi karibuni la vurugu dhidi ya wahamiaji lililowalenga raia wa Nigeria na raia wengine wa Afrika wanaoishi Afrika Kusini.

Ziara ya ujumbe wa Afrika Kusini mjini Abuja ilikuwa sehemu ya juhudi za serikali ya nchi hio kukabiliana na ukosoaji kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kuhusu vurugu dhidi ya wahamiaji.

Mashambulizi yanayochochewa na chuki dhidi ya Waafrika

Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria, Enikanolaiye, alisema kuwa Rais Tinubu aliamuru mkutano huo ufanyike ili kujadili kile ambacho Nigeria imekitaja kuwa ni mashambulizi ya mara kwa mara yanayochochewa na chuki dhidi ya Waafrika nchini Afrika Kusini.

Katika miezi ya hivi karibuni, makundi ya walinzi wa kujichukulia sheria mikononi mwao nchini Afrika Kusini yamewashambulia raia wa kigeni na kupora maduka yanayomilikiwa na wageni mara kadhaa, huku baadhi ya raia wa Afrika Kusini wakiwalaumu wahamiaji kwa matatizo kama uhalifu na ukosefu wa ajira.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, watu wasiopungua wanne wameuawa. Mwezi uliopita, waandamanaji wanaopinga wahamiaji walitaka wahamiaji wasio na nyaraka halali waondoke nchini na waliandamana katika miji kadhaa ya Afrika Kusini.

Maafisa wa Nigeria walisema kuwa tangu kuzuka kwa wimbi la hivi karibuni la vurugu za chuki dhidi ya wageni, raia wa Nigeria wasiopungua 1,490 wamehamishwa kutoka Afrika Kusini na kurejeshwa nchini kwao.

"Tumeona mwenendo ambao sasa umekuwa jambo la kutia wasiwasi kwa serikali ya Nigeria," alisema Enikanolaiye, akiashiria matukio ya vurugu dhidi ya wahamiaji yaliyoanza tangu mwaka 1995.

Alisema kuwa tangu mwaka 2022, raia wa Nigeria wasiopungua 98 wameuawa katika mashambulizi yanayochochewa na chuki dhidi ya wageni.

Uchumi wa Afrika Kusini umestawi zaidi kwa upande wa viwanda barani Afrika, nchi hiyo imevutia wahamiaji kutoka Nigeria pamoja na nchi nyingine kama Ghana, Msumbiji na Malawi. 

Enikanolaiye alisema kuwa si watu wanaoshukiwa kwa uhalifu pekee wanaoshambuliwa, bali pia raia wanaoishi Afrika Kusini na nyaraka halali.

Mwitikio wa serikali

Aliongeza kuwa mamlaka za Nigeria zimerikodi matukio kadhaa ambayo polisi wa Afrika Kusini walionekana kutokuwa tayari kuyazuia haya, jambo lililozua maswali kuhusu uwezekano wa ushiriki au uzembe wa mamlaka za serikali inayodhihirisha kutokuwa tayari au kutokuwa na uwezo wa kuwalinda raia wa kigeni.

Kwa upande wake, Ronald Lamola alisema kuwa serikali ya Rais Cyril Ramaphosa inapinga chuki dhidi ya wageni, ubaguzi wa rangi na aina zote za ubaguzi.

Enikanolaiye amesema kuwa ingawa Nigeria haikubaliani na vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na raia wake walioko nje ya nchi, wanaoshukiwa kufanya makosa wanapaswa kukabiliwa na mchakato wa haki wa kisheria badala ya kushambuliwa na umati.

"Iwapo kuna wahalifu, suluhisho si kuwaua. Wakamateni na wafikisheni mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake."

CHANZO:Reuters