Wizara ya Mambo ya Nje nchini Tanzania imetoa ufafanuzi kuhusu kura iliyopigwa na Kamati ya Bunge la Ulaya kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Ushirikiano wa Maendeleo wa mwaka 2025 kati ya Tanzanai na Umoja huo.
Mapendekezo hayo yaliyopitishwa kwa kura 81, huku kura 1 ikipinga, na kura 4 zikionesha kutokuwa na msimamo, yanataka Umoja wa Ulaya kusitisha msaada wa kifedha kwa Tanzania.
Hata hivyo, uamuzi huo sio wa mwisho, mpaka pale Tume ya Umoja wa Ulaya itakapotoa uamuzi kamili kuhusu mapendekezo hayo.
Aidha mchakato huo bado haujakamilika. Kwa mujibu wa taratibu za Bunge la Umoja wa Ulaya (EU), mapendekezo yanayopitishwa katika ngazi ya kamati lazima baadaye yawasilishwe kwenye Kikao Kikuu cha Bunge la Ulaya, kinachojumuisha wanachama zaidi ya 700, kwa ajili ya kujadiliwa na kufanyiwa uamuzi.
“Ni muhimu kufahamu kwamba uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na nchi washirika wake, ikiwemo Tanzania, unaendeshwa kupitia Tume ya Ulaya, ambayo ndiyo chombo cha utendaji cha Umoja huo. Kama ilivyo katika mifumo mingi ya kibunge, mapendekezo yanayopitishwa na kamati za kibunge au na Bunge lenyewe huwasilishwa kwa taasisi husika za kiutendaji kwa ajili ya kuzingatiwa na kufanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa,” imesema sehemu ya taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania.
Wakati huo huo, Wizara imesema kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya unaendelea kuimarika, na unazidi kustawi kwa misingi ya kuheshimiana.
Hatua hii inafuatia kuwepo kwa malalamiko kutoka kamati za haki za binadamu za EU kuhusu hali ya kisiasa nchini Tanzania, hasa baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Tume ya Uchunguzi ya Matukio ya Oktoba 29, iliyowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 23, 2026, imeonesha watu 518 walipoteza maisha katika vurugu za baada ya uchaguzi. Hata hivyo, baadhi ya vyanzo ikiwemo wanaharakati wanadai idadi ya waliofariki ni zaidi ya iliyotajwa na Tume.




















