Tanzania: Mwigulu Nchemba aagiza hatua za haraka kuchukuliwa baada ya tukio la moto
Jumla ya vibanda 500 vya wafanyabiashara wadogo viliteketea katika tukio hilo.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwigulu Nchemba ameagiza kuchukuliwa hatua za haraka, ili kurejesha shughuli za biashara kwenye eneo la Soko la Mawasiliano, jijini Dar es Salaam.
Agizo hilo linafuatia tukio la moto ulioteketeza soko hilo, Aprili 4, 2026.
Kulingana na Nchemba, serikali ya nchi hiyo inaendelea kufuatilia kwa karibu tukio hilo, akisema kuwa itatoa kauli rasmi baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa kina.
“Mheshimiwa Rais amepata taarifa ya jambo hili, anawapa pole sana na ameelekeza uchunguzi wa kina ufanyike ili tujue chanzo cha tatizo hili. Na kazi hiyo imekwisha kuanza ili tuweze kupata undani wa chanzo cha jambo hili lililojitokeza,” alisema Nchemba alipokagua soko hilo Aprili 6, 2026.
Aidha, Nchemba ameagiza eneo la soko hilo kusafishwa mara moja ili kuruhusu wafanyabiashara kuanza taratibu za kurejesha shughuli zao.
“Mkurugenzi, ukitoka hapa leo wakati unamalizia siku… kesho hapa pote pasafishwe. Hii kazi ya kusafisha kesho iishe,” aliagiza.
Jumla ya vibanda 500 vya wafanyabiashara wadogo viliteketea katika tukio hilo.
Nchemba aliongeza kuwa serikali ya nchi hiyo itashirikiana na taasisi za kifedha kusaidia wafanyabiashara wenye mikopo waliopoteza mitaji yao, pamoja na kuweka utaratibu wa kuwaongezea muda wa kurejesha mikopo hiyo na kuwezesha upatikanaji wa mikopo mipya yenye nafuu kupitia mamlaka za serikali za mitaa.