Umoja wa Afrika yasema Tanzania ilikiuka misingi ya demokrasia katika Uchaguzi Mkuu

Umoja wa Afrika imesema Tanzania inatakiwa kuyapa kipaumbele masuala ya mageuzi ya uchaguzi na siasa ili kushughulikia chanzo cha changamoto zake za kidemokrasia zilizoibuka katika mchakato wa uchaguzi

By
Ujumbe uliongozwa na rais wa zamani wa Botswana Mokgweetsi E.K. Masisi

Uchaguzi wa Tanzania haukufuata misingi ya kidemokrasia, ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Afrika ulisema Jumatano kuhusu kura hiyo yenye utata ambayo ilisababisha maandamano mabaya.

Ujumbe wa uangalizi wa AU uliongozwa na Mokgweetsi Masisi, Rais wa zamani wa Botswana, akisaidiwa na Geoffrey Onyeama, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria.

Ujumbe huo ulijumuisha waangalizi 72 waliotoka katika mataifa mbalimbali ya Afrika.

Rais Samia Suluhu Hassan alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 29, lakini wapinzani waliishtumu serikali kwa udanganyifu na kukaibuka maandamano kutokana na kutengwa kwa wapinzani wake wakuu.

"Katika hatua hii ya awali, Ujumbe wa AU umejiridhisha kuwa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa 2025 haukufuata utaratibu wa AU, mifumo ya kanuni, na majukumu na viwango vingine vya kimataifa vya uchaguzi wa kidemokrasia," ujumbe huo ulisema.

Waangalizi waliona kura zikijaa katika vituo kadhaa vya kupigia kura, huku watu wakipewa karatasi nyingi za kupiga kura, ilisema, pia ikibaini kutokuwepo kwa mawakala wa vyama vya siasa.

Wakati wa kuhesabu, waangalizi wengine walitakiwa kuondoka kwenye vituo, iliongeza.

Serikali ya Tanzania inasema uchaguzi ulikuwa wa huru na haki.

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA, ambacho kilizuiwa kushiriki uchaguzi huo, kinasema kuwa kimekusanya taarifa za mamia ya vifo wakati wa maandamano hayo.

Boniface Mwabukusi, rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika anayewakilisha wanasheria Tanzania Bara, alisema anakadiria idadi ya waliofariki kuwa zaidi ya 1,000 kutokana na ripoti kutoka kwa watu wa ndani.

Kukusanya hesabu halisi ilikuwa ngumu, hata hivyo, kwa sababu serikali ilikuwa inatishia watu kutoa taarifa, alisema.

Rais Samia, ambaye aliapishwa kwa muhula mwingine Jumatatu baada ya matokeo rasmi kumtangaza alipata asilimia 98 ya kura, alikiri kuwa watu walifariki, lakini serikali yake imewataja wapinzani kuwa wameongeza chumvi sana.

"Tanzania inatakiwa kuyapa kipaumbele masuala ya mageuzi ya uchaguzi na siasa ili kushughulikia chanzo cha changamoto zake za kidemokrasia zilizoibuka katika mchakato wa uchaguzi kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa wiki iliyopita," ujumbe wa AU uliongeza katika taarifa yake.