Simba Sports Club ya Tanzania 'yamtimua' Dimitar Pantev
Pantev alichukua mikoba ya kuwafundisha ‘Wekundu wa Msimbazi’ mwezi Oktoba 2025, akitokea Gaborone United ya Botswana.
Klabu ya soka ya Tanzania, Simba imesitisha mkataba na aliyekuwa meneja mkuu Dimitar Pantev pamoja na wasaidizi wake wawili.
Kulingana kwa taarifa ya umma iliyotolewa na Simba Sports Club kupitia ukurasa wake wa X (zamani twitter), Simba imefikia makubaliano hayo ya pande mbili, huku kikosi hicho sasa kikiwa chini ya kocha Selemani Matola, wakati mchakato wa kutafuta kocha mwingine ukiendelea.
Uamuzi huo unakuja siku mbili baada ya Simba Sports Club kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Stade Malien ya Mali, katika mchezo Kundi D wa Ligi ya Mabingwa Afrika, uliofanyika Novemba 30 mjini Bamako.
Kabla ya hapo, timu hiyo ilipoteza nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya Petro de Luanda ya nchini Angola.
Pantev alichukua mikoba ya kuwafundisha ‘Wekundu wa Msimbazi’ mwezi Oktoba 2025, akitokea Gaborone United ya Botswana.
Raia huyo wa Bulgaria alirithi mikoba iliyoachwa wazi na Fadlu davids aliyetimkia Raja Casablanca ya Morocco.